2012-11-26 08:41:46

Kazi inapata chimbuko lake ndani ya Familia na ni kwa ajili ya Familia


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu tena tuendelee na tafakari yetu ya kazi na familia. Na kwa namna ya pekee leo tukumbushane kuwa kazi ni kwa ajili ya manufaa ya familia. Lakini, pia kazi inapata chimbuko lake katika familia. RealAudioMP3
Kila mmoja anajua kuwa kazi ni kwa ajili ya familia kwani kila mtu anayefanya kazi analengo la kuiwezesha familia yake kufurahia matunda ya hiyo kazi yake. Wazazi wanapofanya kazi na hasa ya malezi wana lengo la kufurahia makuzi na baadaye ya watoto wao.
Hapa ni vizuri tukumbushane kuwa, endapo mmoja wa wanafamilia hatatimiza majukumu yake vizuri basi familia hiyo itaendelea kuwa na mapungufu mengi ya kimalezi, kijamii, kimahusiano au hata kiuchumi.
Lakini pia kazi ina chimbuko lake katika familia kwani kazi ni wito au wajibu ambao mwanadamu ameupokea toka kwa Mungu. Hivyo mwanadamu anapofanya kazi anajibu wito alioupokea toka kwa Mungu lakini kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya ya watu na familia ikiwa ndiyo jumuiya ya kwanza.
Mwanadamu hapaswi kufanya kazi tu kwa ajili ya faida yake binafsi bali akiwa anafahamu fika kuwa amekabithiwa jumuiya inayomuhitaji ashirikishe vipaji vyake hivyo kutushirikisha vipaji vyake kwa ajili ya jumuiya hii ni kuikosea haki.
Ni vizuri tukumbushane kuwa kazi ambayo chimbuko lake ni familia na kwa ajili ya familia haiishii kwenye familia tu, bali, inapanuka na kuigusa jamii nzima. Inagusa pia mfumo mzima wa uchumi. Ndio sababu uchumi ulio imara lazima uwe na mlingano sahihi na maisha ya jamii nzima na sio mwanadamu kugeuzwa kuwa chombo cha ukandamizaji na uzalishaji usio na faida kwake. Kipimo cha mfumo wa uchumi kisitegemee tu soko bali bali mahusiano ya kibinadamu aliyeko kwenye mazingira fulani, mwenye utamaduni, lugha na historia fulani.
Mwanadamu mwenye vionjo na anayeguswa na matukio ya maisha kama ya furaha na uchungu. Kwa wakati wote tutambue kuwa kazi, uchumi na mahusiano ya kibinadamu havitenganishwi. Tunapovitenganisha tuna kataa ukweli kuwa kazi imetokana na mwanadamu na ni kwa ajili ya mwanadamu na si vinginevyo.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano- Roma.









All the contents on this site are copyrighted ©.