Waamini wa Kanisa Katoliki Afrika ya Kaskazini ni wachache lakini: ni mashahidi wa
majadiliano, huduma, sala na mang'amuzi mbali mbali ya maisha!
Baraza la Maaskofu Katoliki Kanda ya Afrika ya Kaskazini, CERNA, limehitimisha mkutano
wake wa mwaka, uliofanyika Jimboni Mazara del Vallo, Sicilia, Kusini mwa Italia, kwa
mwaliko wa Askofu Domenico Mogavero.
Maaskofu hao wamekazia umuhimu wa kuendeleza
na kudumisha majadiliano ya kitamaduni kwa watu wanaoishi katika Ukanda wa Mediterrania;
kinzani na migogoro inayoendelea kuhatarisha haki, amani na usalama huko Mashariki
ya Kati, tatizo la uhamiaji na misimamo mikali ya kidini; mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa
kwa umakini mkubwa, kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Afrika ya Kaskazini.
Maaskofu
wanatambua kwamba, Waamini wa Kanisa Katoliki ni wachache Kaskazini mwa Afrika, lakini
ni kielelezo makini cha ushuhuda, majadiliano ya kina, huduma, maisha ya sala na mang'amuzi
mbali mbali yanayopata chimbuko lake kutoka katika eneo hili. Maaskofu wamejadili
na kutoa mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto
wadogo, bila kusahau tatizo la wahamiaji ambalo linaendelea kuongezeka siku hadi siku
kutokana na kinzani na vita huko Mashariki ya Kati.
Makanisa ya Kaskazini
mwa Afrika yana idadi kubwa ya waamini wahamiaji wanaotoka Kusini mwa Jangwa la Sahara
kwa sababu mbali mbali, lakini wengi wao ni wale ambao wako njiani kuelea Ulaya kupitia
Sicilia. Ni kundi la watu wanaokabiliana na changamoto na hali ngumu katika maisha
yao, anasema Askofu Domenico Mogavero.
Tofauti za kidini na kitamaduni zisiwe
ni sababu ya choko choko na kinzani za kijamii, bali utajiri unaowawezesha watu kuvumiliana,
kushirikiana na kutolea ushuhuda wa tunu msingi za kijamii na kidini zinazowaunganisha
badala ya kila upande kung'ang'ania na kuendelea kushikilia mambo madogo madogo yanayowagawanya!
Bado kuna ubaguzi unafanywa kwa misingi ya kidini, kwani kwa Wakristo wanaoishi
Kaskazini mwa Afrika wanadhaniwa kwamba, ni raia wa daraja la pili na hawana haki
sawa na wananchi wengine wenye imani tofauti na ile ya kwao. Ubaguzi huu unafanyika
hata katika sheria za nchi, kwani hakuna uhuru wa dhamiri.