Chuo Kikuu cha Dodoma kinavyojipanga kupunguza gharama za matibabu ya ugonjwa wa figo!
Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, ameishauri Serikali kupanga
utaratibu utakaosaidia wagonjwa wa figo kumudu gharama za matibabu pindi huduma hiyo
itakapoanza kutolewa Januari mwakani na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mkapa
ametoa ushauri huo Ijumaa tarehe 23 Novemba 2012, wakati alipotembelea chuo hicho,
kukagua mashine za kisasa 10 za kusafisha damu zilizotolewa na Serikali ya Japan
kupitia Mfuko wa Benjamin. Amesema, kutokana na uchumi walionao Watanzania wa kawaida
hawataweza kumudu kulipia gharama za matibabu hizo kwa kuwa ni ghali sana .
Kwa
kuwa hospitali zinazotoa matibabu hayo hapa nchini ni chache hivyo hospitali hiyo
ijiandae kuwapokea wangonjwa wengi kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi. Akizungumzia
kuhusiana na msaada wa mashine hizo, Mkapa amesema awali taasisi yake iliomba msaada
wa mashine hizo kutoka Japan kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wa Chuo Kikuu
hicho ili waweze kujifunza kuwatibu wagonjwa hao. Hata hivyo, amesema kutokana na
mahitaji ya chuo hicho wamebaini ni vema wakaongeza idadi ya wataalam hao.
Naye
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Noah Chihoma, amesema Chuo hicho kilipeleka wafanyakazi
sita nchini Japan kujifunza jinsi ya kutumia mashine hizo za kisasa za kusafisha
damu. Dk. Chihoma amesema kwa sasa mashine hizo hazijaanza kutumika kwa sababu bado
wanasubiri wataalamu wa kutoka kampuni nchini Japan ili waweze kufanya uhakiki wa
mwisho ili zianze kutumika.
Amesema pamoja na wataalamu hao sita kutoka hospitali
yao, watashirikiana na wataalamu wengine kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili
kuweza kuziendesha mashine hizo. Dk. Chihoma amesema kwa sasa hivi hospitali yao
pamoja na kutibu magonjwa ya kawaida kwa wafanyakazi na wanafunzi, pia kinatoa matibabu
kwa Jamii inayokizunguka chuo hicho.