Baba Mtakatifu Benedikto XVI ametimiza ahadi yake!
Kitabu cha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuhusu Simulizi za Utoto wa Yesu,
kimekuja kwa wakati muafaka, ili kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema kufanya
tafakari ya kina hasa wakati wa Kipindi cha Majilio na Noeli, kinachotoa fursa maalum
kwa ajili ya kuzama katika utamaduni wa Biblia; tafakari za kitaalimungu na maisha
ya kiroho.
Baba Mtakatifu ametimiza ahadi ambayo alikuwa amejiwekea mwenyewe
tangu alipochapisha kitabu chake cha kwanza kuhusu Yesu wa Nazareti, kinachofafanua
kuhusu maisha ya Yesu hadharani; Kitabu cha Pili akazama zaidi katika Mateso na Ufufuko
wa Yesu. Alikwisha sema wazi kwamba, lengo la kazi yake ni kuwasaidia waamini na watu
wenye mapenzi mema, kuweza kumfaham zaidi Yesu; ujumbe na utekelezaji wa utume wake
hapa duniani. Ndiyo maana aliacha kwa makusudi mazima, Simulizi za Maisha ya Utoto
wa Yesu, ingawa aliweza kuwaonjesha wasomaji wake kidogo kuhusu maisha ya Utoto wa
Yesu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatambua kwa unyenyekevu mkubwa
kwamba, licha ya mapungufu yanayoweza kujitokeza katika kitabu hiki, lakini jambo
la msingi ni kusaidia kujenga majadiliano ya kina kwa kuangalia yaliyopita, yaliyopo
na yale yanayokuja kama hija ya watu kumwendea Yesu Kristo, ili kuandamana naye.
Ndivyo
anavyoandika Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwenye tahariri yake
juma hili, inayojikita katika ahadi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, kutaka kuandika kitabu maalum kitakachogusa Simulizi za Utoto wa Yesu, ahadi
hii sasa imetimia, kazi ni kwako mwamini. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, katika
uzee wake, alijikita zaidi katika tafakari iliyoandikwa kwa mtindo wa shahiri juu
ya "Utatu wa Roma".
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amejitahidi kuwasaidia
watu wanaoutafuta uso wa Yesu ili kukutana naye. Alitambua vikwazo ambavyo vilikuwa
mbele yake, vya kweli au kinzani zinazojitokeza katika tafakari ya kina katika Maandiko
Matakatifu, Taalimungu, Utamaduni wa mwanadamu pamoja na kinzani binafsi.
Padre
Lombardi anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ameng'amua
kwanza kabisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, jinsi ambavyo watu walijitahidi kumtofautisha
Yesu wa historia na Yesu wa Imani. Amejibidisha kutoa mwelekeo wenye utulivu unaopania
kujenga na kuimarisha urafiki binafsi na Yesu, huduma makini kwa viongozi wa Kanisa.
Anatambua dhamana yake ya kulinda na kutetea Imani ya Kanisa.
Padre Lombardi,
anachukua nafasi hii kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuweza
kuhitimisha kazi kubwa ambayo imedumu kwa takribani miaka tisa. Hayati Kardinali Martini
alipokuwa anahitimisha uzinduzi wa kitabu cha kwanza alisema kwa hakika, kitabu hiki
ni kizuri, kinatusaidia kumfahamu Yesu Mwana wa Mungu na imani kubwa ya mtunzi wa
kitabu hiki.