YESU KRISTO MFALME WA ULIMWENGU NDIYE MLANGO WA IMANI
Tunakuleteeni habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja ujumbe wa Neno aliyefanyika
mwili, Mfalme wa mbingu na nchi. Ni Dominika ya 34 ya mwaka B iliyo pia Sherehe ya
Yesu Kristu Mfalme.
Kanisa linashangilia
na kusherehekea utukufu wa Mwana wa Mungu, Yesu Kristo Mfalme. Kanisa linatangaza
daima utawala na enzi ni vya Yesu Kristu mfalme na hivi lajiweka chini ya uongozi
wake aliye kichwa na mwanga katika safari ya kuelekea mbinguni. Pamoja na tangazo
hilo Kanisa latuhimiza kumfuata Yesu Kristu mfalme, kukiri ukuu wake wazi wazi machoni
pa mataifa lililo hasa lengo la sherehe hii.
Nabii Ezekieli anatupa picha halisi
ya mfalme aliye pia mchungaji mwema, aliye kinyume na wafalme wa dunia. Mchungaji
wa kondoo anayetabiriwa na Ezekieli ni yule ambaye anatafuta kundi lake lililopotea
na kulirudisha katika malisho safi na baadaye kulisalimisha pia nyumbani.
Kundi
hili la kondoo ni wagonjwa, waliopotea waliovunjika moyo na waliofukuzwa. Picha hii
ya mchungaji inajitokeza katika Yesu Kristu mfalme ambaye kwa njia ya msalaba watu
wote wamerudishwa nyumbani. Kumbuka maneno yake alipokuwa akizungumza na Nikodemo
“kama vile Musa alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani naye mwana wa mtu atainuliwa
juu vivyohivyo ili kila anayemwamini awe na uhai wa milele” Yn 3:14-15.
Katika
somo la pili mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho anatualika kusadiki kuwa Kristu ndiye
limbuko letu. Ndiye ambaye amebatilisha kifo kwa njia ya msalaba wa ushindi. Anaonesha
ufalme na ukuu wake kwa kushinda kifo kilicholetwa duniani kwa njia ya Adamu. Kwa
ushindi dhidi ya kifo Mungu amemtukuza na kumwadhimisha mno, na hivi mwishoni mwa
dunia utawala wa shetani utashindwa kabisa. Mtume Paulo hatangazi jambo jingine bali
kuwa Yesu Kristo ni Mfalme ambaye Kanisa lamshangilia nakumtukuza kwa shangwe na vigelegele.
Sisi wanakanisa tunapaswa kufuata mtililiko huohuo pasipo mashaka tukitangaza ushindi
wa Bwana.
Mwinjili Mathayo anatuonesha mfalme mwenye mamlaka juu ya mbingu
na dunia, mwenye uwezo wa kutoa hukumu kadiri ya upendo na haki. Mfalme huyu ameketi
katika kiti cha enzi akiwabagua mataifa yote, wengine mkono wa kulia na wengine mkono
wa kushoto. Ndiyo kusema kwanza ana enzi na mamlaka lakini pia ana haki.
Katika
hukumu anayotoa yapo mambo msingi ambayo anayatazama. Kama mmoja aliwalisha maskini
au hapana, kama mmoja aliwatazama wagonjwa ambao ni kielelezo cha uwapo wa sauti ya
Mungu katikati ya jumuiya ya watu. Kigezo kingine ni kile cha kuwatazama wafungwa
kifungoni, walio utumwani na wenye njaa. Kwa wale ambao waliwahudumia hawa wahitaji
atawaambia kaeni mkono wa kulia na mkapate kula vilivyo vya Baba yangu maana nilipokuwa
mgonjwa mlikuja kuniona hospitali. Kumbuka kuwa mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu.
Kwa hakika ukitazama vema lengo la ainisho hili la watu mbalimbali waliowahitaji,
utagundua nguzo kuu ili mmoja aweze kuingia katika ufalme wa Mbinguni ni MAPENDO KWA
JIRANI NA KWA MUNGU. Ni kushuhudia kwa dhati IMANI Katoliki, imani tendaji, imani
inayokuza ubatizo hadi mwisho wa nyakati. Ni kubaki katika pendo la Mwana wa Mungu
katika kuhudumu waliowake.
Mpendwa tunaposherehekea Sherehe ya Mfalme wetu
tukumbuke kuwa yeye anapaswa kutawala katika familia zetu zote, katika maneno yetu
na matendo yetu. Maneno kama “ mteja ni mfalme” yafaa kuangaliwa vizuri kama kweli
yanakuza ufalme wa Kristu au ufalme wetu sisi wenyewe!
Tunawatakieni heri
na baraka Waamini wote na zaidi wale ambao parokia zao na makanisa yao yako chini
ya somo Yesu Kristo Mfalme. Mkashike imani na mtoe mfano wa kuigwa mkiongozwa na Yesu
Kristu mfalme wa Amani. Tumsifu Yesu Kristo Mfalme.
Tafakari hii imeletwa kwako
na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.