2012-11-22 10:40:34

Wasanii changieni karama na utajiri wenu kuhusu imani kwa Yesu Kristo, sura na kielelezo cha utukufu wa Mungu unaoangaza historia ya mwanadamu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano, tarehe 21 Novemba 2012 amemtumia ujumbe wa matashi mema Kardinali Gianfranco Ravas, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, kama sehemu ya hitimisho la mkutano wa kumi na saba wa hadhara uliofanywa na taasisi za kipapa, uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu "Msaniii kama Kanisa, shahidi wa uzuri wa imani.

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu ambao umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, anawapongeza kwanza kabisa viongozi wa Taasisi ya Kipapa ya Lugha ya Kilatini aliyoianzisha hivi karibuni kwa kumteuwa Profesa Ivano Dionigi kuwa Rais wake wa kwanza.

Ni matumaini yake kwamba, Taasisi hii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu na utamaduni watakoleza moyo na hamu ya watu kupenda kujifunza lugha ya Kilatini, ambao ni utajiri na urithi mkubwa wa kitamaduni unaopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni ameamua pia kuunganisha Tume ya Mali za Kitamaduni za Kanisa kuwa chini ya Baraza la Kipapa la Utamaduni, kwani ni masuala yanayolandana kwa karibu zaidi na nyenzo muhimu katika mwingiliano kati ya Imani ya Kikristo na binadamu.

Mkutano huu umefanyika wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani na kwamba, mada iliyochaguliwa ni kielelezo makini cha changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kuwataka Wasanii kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya karama na vipaji vyao.

Hii ndiyo dhamana endelevu ya majadiliano na mshikamano na wasanii kama alivyobainisha pia Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili katika Waraka wake kwa Wasanii wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya Miaka elfu mbili ya Ukristo. Mama Kanisa anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anapenda kuhakikisha kwamba, Wasanii wanapewa nafasi na dhamana yao katika Jumuiya ya Waamini, Jamii inayowazunguka na katika ulimwengu wa Wasanii, ili kuendelea kuchangia karama na utajiri wao kuhusu uzuri wa imani sanjari na kuendeleza uzuri wa dunia, kama walivyobainisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Ni wajibu wa Wasanii kugundua uzuri wa imani, kuuelezea na kuutangaza kwa kutumia lugha yao ya kisanii, kwani wao kimsingi, ni mashahidi wa uzuri wa imani, wanaoweza kuchangia katika wito na utume wa Kanisa kwa njia ya kazi zao za sanaa zinazojionesha kwa namna ya pekee katika Ibada za Kanisa. Sanaa takatifu anasema Baba Mtakatifu inalenga kuelezea matendo makuu ya Mungu, hata katika umaskini wake, mwaliko wa kuziangalia kazi hizi kwa macho ya taamuli.

Msanii mwamini ndani yake anaonesha imani, moyo wa sala, tamaa ya ndani na hali ya kukesha katika ukimya, akitekeleza mapenzi ya Mungu, daima akisubiria kuiona Pentekosti yake. Ni kazi inayowaunganisha waamini na Kristo mwenyewe.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu anachukua fursa hii, kuwaalika Wasanii waamini na wote wanaotamaduni kudumisha majadiliano ya Imani, kuhakikisha kwamba, wanafanya hija ya maisha na utume wao kushuhudia uzuri wa imani kwa Yesu Kristo, sura na kielelezo cha utukufu wa Mungu unaoiangazia historia ya binadamu.

Ili kukuza na kudumisha vipaji vya wasanii vijana, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alitoa tuzo kwa washindi kadhaa waliofanya vizuri katika medani zao. Anawaweka wasanii wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, kielelezo cha imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.