Rais Michel Joseph Martelly wa Haiti akutana na Papa Benedikto XVI mjini Vatican
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Alhamisi, tarehe 22 Novemba 2012, amekutana
na kuzungumza na Rais Michel Joseph Martelly wa Haiti, na badaye, ujumbe wake umekutana
pia na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, aliyeongoza ujumbe wa Vatican
katika mazungumzo hayo.
Viongozi wa pande hizi mbili wamezungumzia uhusiano
mwema uliopo kati ya Vatican na Haiti. Wamejadili kwa namna ya pekee, mchango wa Kanisa
nchini Haiti kupitia Mashirika yake ya misaada hasa katika sekta ya elimu, afya na
huduma ya maendeleo endelevu kwa Jamii.
Rais wa Haiti amelishukuru Kanisa
kwa jitihada za kufufua hali ya nchi hiyo iliyokuwa imeharibika vibaya baada ya kukumbwa
na tetemeko la ardhi. Viongozi hawa wawili wanapania kwa pamoja kuendeleza ushirikiano
baina ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Haiti.