Papa asikitishwa na mashambulizi ya kivita yanayoendelea Ukanda wa Ghaza
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano, tarehe 21 Novemba 2012 baada ya
Katekesi yake, ameonesha masikitiko makubwa kutokana na mashambulizi yanayoendelea
kutokea huko Mashariki ya Kati. Anasema, anafuatilia matukio haya yote kwa wasi wasi
na hofu kubwa kutokana na kuongeza kwa mashambulizi kati ya Israeli na Palestina,
kwenye Ukanda wa Ghaza. Pamoja na kuendelea kusali, lakini anawajibika kukumbushia
kwamba, vurugu na visisasi si suluhu ya matatizo wanayokabiliana nayo.
Baba
Mtakatifu anapenda kutumia nafasi hii kuwaalika viongozi wa pande hizi mbili kurudi
tena katika meza ya majadiliano, itakayositisha vita. Anawahimiza viongozi wa pande
hizi mbili kutekeleza maamuzi ambayo yatasaidia kulinda na kudumisha amani ili kuondokana
na mgogoro wa vita na hatimaye, kujikita katika jitihada zinazopania kudumisha amani
na upatanisho.