2012-11-22 09:12:58

Mikakati ya maboresho ya maisha na hali ya kazi ya mabaharia duniani; uharamia na changamoto zake!


Wajumbe wa Kongamano la ishirini na tatu juu ya Utume wa Bahari, lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hapa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 22 Novemba, 2012, wanaendelea kuchambua madhara yanayosababishwa na maharamia baharini pamoja na hali ya maisha ya mabaharia na familia zao wanaokumbana na mikasa kama hii.

Vitendo vya uharamia vimeongezeka kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi, na kwenye nchi zinazounda Pembe ya Afrika. Usalama wa maisha ya mabaharia na mali wanazobeba uko mashakani, hali inayopelekea pia kuongezeka kwa gharama za usafirishaji.

Itakumbukwa kwamba, Kongamano hili kwa namna ya pekee, linapania kukoleza juhudi za Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa mabaharia kwani Habari Njema ya Wokovu inapasa kumgusa kila mtu mahali alipo na katika utume wake, kama alivyobainisha Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya, wakati akichangia mada juu ya Uinjilishaji Mpya katika Ulimwengu wa Mabaharia.

Shirika la Kazi Duniani, ILO baada ya kazi kubwa ya miaka saba, hatimaye, kuanzia mwaka 2013 kutakuwa na chombo madhubuti kinachopania kuboresha maisha na hali ya kazi kwa mabaharia zaidi ya millioni moja na laki mbili, wanaotekeleza kazi yao sehemu mbali mbali za dunia.

Serikali zitapaswa kuhakikisha kwamba, katika bandari zao kuna msaada wa kisheria, utakaorahisisha mabaharia kupata huduma za kijamii, matibabu, chakula, mahali pa kufanyia michezo pamoja na fursa ya kuwasiliana na familia zao. Mabaharia pia watapatiwa fursa ya kushiriki katika maisha ya kiroho ya dini zao wanapokuwa bandarini.

Wajumbe wa kongamano hili wanasema kwamba, uharamia kwa sasa ni tatizo nyeti, linaloendelea kukuza na kupanuka kwa kasi kubwa hasa kwenye Bahari ya Hindi, ingawa uharamia huu unafanyika kwa malengo na mifumo mbali mbali. Baadhi ya wajumbe, wametoa ushuhuda wa jinsi ambavyo kwa miaka mingi wamekuwa wakijihusisha na majadiliano kati ya mabaharia na maharamia; majadiliano ambayo yamewezesha Mabaharia na meli zao kuachiwa huru ili kuendelea na safari zao.

Mabaharia wakati mwingine wanashikiliwa mateka kwa kipindi kirefu, hali ambayo inasababisha usumbufu mkubwa, baadhi ya mabaharia waliotekwa wanashuhudia kwamba, kipindi chote hiki kwao imekuwa ni Njia ya Msalaba, wamekitumia kwa ajili ya kusali zaidi, kwani daima waliyaona maisha yao kuwa hatarini.

Wajumbe wamezungumzia pia dhamana na nafasi ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwa mabaharia, kama utume wa Mama Kanisa kwa mabaharia ili kukidhi kiu ya maisha yao ya kiroho. Huu ni ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Mama Kanisa tangu Mwaka 1930 amekuwa bega kwa bega na mabaharia katika safari zao baharini, daima akiwaonesha dira ya matumaini katika furaha, shida na mahangaiko yao ya ndani. Meli za abiria ni jukwaa linaloweza kutumiwa na Mama Kanisa katika azma ya Uinjilishaji Mpya.









All the contents on this site are copyrighted ©.