Takwimu za kimataifa zinabainisha kwamba, kuna jumla ya wafanyakazi milioni thelathini,
wanaotekeleza wajibu wao katika sekta ya uvuvi sehemu mbali mbali duniani. Lakini
hii ni sekta ambayo inasemekana kuwa ni hatari sana, ikilinganishwa na kazi nyingine
zozote, kwani wavuvi wamekuwa wakikumbana na nyanyaso, dhuluma na ma teso ya kila
aina, wanapotekeleza wajibu wao, ili kuhakikisha kwamba, mamillioni ya watu wanapata
samaki safi na salama kwa ajili ya kitoweo.
Inakadiriwa kwamba, asilimia kumi
na tatu ya wavuvi wote duniani ni watu wanaokabiliana na hatari kubwa zaidi katika
maisha yao. Hali hii ni mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea duniani, kwani wanakabiliwa
na hatari kubwa ya kifo, ikilinganishwa na wavuvi kutoka katika nchi zilizoendelea
zaidi duniani.
Yote haya yanajadiliwa kwa namna ya pekee na wajumbe wanaohudhuria
Kongamano la ishirini na tatu la kimataifa la Utume wa Bahari lililoandaliwa na Baraza
la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum,
inayoendelea hapa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, kila mwaka ifikapo targhe 21
Novemba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wavuvi Duniani.
Lengo la
Utume wa Bahari ni kuhakikisha kwamba, hata ulimwengu wa mabaharia unashiriki kikamilifu
katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya; changamoto endelevu inayofanyiwa kazi na Mama
Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Mwakilishi wa Shirika
la Kazi Duniani, ILO amezungumzia kuhusu Mkataba wa Shirika hilo namba 188 unaozungumzia
kuhusu sekta ya uvuvi duniani. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hadi leo hii,
Mkataba huu haujapata idadi kubwa ya nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani wanaouunga
mkono, kiasi cha kushindwa kutekelezwa na nchi wanachama. Wanachama wa Utume wa Bahari
kwa kushirikiana na watu wanaojitolea wanaendelea kuzihamasisha nchi wanachama wa
ILO, kuridhia Mkataba huu, ili uweze kuwa ni sheria.
Sekta ya uvuvi imegawanyika
katika makundi makuu matatu: uvuvi wa kujikimu, uvuvi wa soko mahalia na uvuvi wa
kimataifa. Wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wametoa ushuhuda unaonesha
utawala bora katika sekta ya uvuvi sanjari na kulishirikisha Kanisa katika maisha
na utume wa wavuvi, jambo ambalo bado liko nyuma sana kwa nchi nyingi za Kiafrika.
Lakini, ikumbukwe kwamba, ni kundi ambalo linakabiliana na hatari kubwa katika maisha
yake, hivyo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa
kwa kukazia Utume wa Bahari mahali ambapo bado haujaanzishwa.
Kutoka nchini
Angola, Utume wa Bahari unaonesha kuzaa matunda mazuri kutokana na ushirikiano uliopo
kati ya Kanisa na Jumuiya ya Wavuvi wanaoishi Angola na Sao Tomè. Wanaendelea kuandamana
na Jumuiya ya wavuvi katika mahitaji yao ya kijamii na kiroho pamoja na kujiunga nao
wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wavuvi, ili kutambua kwamba, Kanisa linawathamini
na linataka kuwaenzi, licha ya changamoto na kinzani mbali mbali wanazokabiliana nazo
katika utume wao. Utume wa Bahari umekuwa ni msaada mkubwa katika mapambano dhidi
ya Ukimwi, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ulevi wa kupindukia.
Wahamasishaji
wa kongamano hili wanasema kwamba, hata wavuvi wanapaswa kutangaziwa Habari Njema
ya Wokovu, kwa kuzinagatia: mazingira na mahitaji ya watu wanaofanya kazi katika sekta
ya uvuvi. Wafundishwe Biblia, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii
ya Kanisa bila kusahau maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa. Familia za wavuvi zisaidiwe
kukabiliana na changamoto za maisha kwa imani na matumaini. Maadhimisho ya Mwaka wa
Imani, yatoe changamoto kwa Mama Kanisa kuwawezesha wavuvi kuzima kiu ya maisha yao
ya kiroho.