2012-11-21 08:41:53

Seminari na taasisi za elimu ya juu nchini Burundi zinaalikwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani


Askofu Bonaventura Nahimana wa Jimbo Katoliki Rutana anazialika seminari, nyumba za malezi pamoja na taasisi za elimu ya juu nchini Burundi kuhakikisha kwamba, zinashiriki kikamilifu katika kuhamasisha maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hivi karibuni.

Askofu Nahimana ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa kuzindua Mwaka wa Masomo kwa Seminari kuu ya Falsafa ya “St. Cure d’Ars”, iliyoko Jimbo kuu la Bujumbura, Burundi, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na Padre Emmanuel Gihutu, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu katoliki Burundi kuwa Gombera mpya wa Seminari hiyo.

Askofu Nahimana ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Elimu Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi, anasema, maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanapaswa kuacha chapa ya kudumu hata katika masomo na maisha ya Majandokasisi pamoja na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini humo. Vijana wajitahidi kuishi kikamilifu imani yao, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mguso, wakitambua kwamba, wao ni wafuasi wa Kristo, kumbe wanadhamana na wajibu wa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao manyofu na adili.

Askofu Nahimana ametumia fursa ya maadhimisho hayo kutangaza kwamba, hapo targhe 8 Desemba 2012 wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi, litafungua Seminari kuu mpya ya taalimungu ya Kiryama, Jimboni Bururi. Hii itakuwa ni Seminari kuu ya nne, kati ya Seminari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi. Itakuwa ni Seminari kuu ya pili kutoa majiundo ya kitaalimungu.

Hizi ni dalili za neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kuongezeka kwa miito ya Kipadre nchini Burundi, lakini waamini wanakumbushwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea miito kwani mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kanisa linawahitaji watenda kazi wengi, watakatifu na wachapakazi, watakaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.