Mwaka wa Imani uimarishe Imani kwa Kristo na Kanisa lake!
Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi, hivi karibuni wakati wa
maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa ajili ya Mashirika ya Kipapa ya Utoto
Mtakatifu, amewaalika waamini nchini Kenya kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema maadhimisho
ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ili kuimarisha
imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Kardinali Njue anasema, Mwaka wa Imani
ni kipindi cha neema na wakati uliokubalika kwa waamini kuweza kuimarisha imani, matumaini
na mapendo. Huu ni utume endelevu wa Mama Kanisa ambao kila mwamini anapaswa kuushiriki
kikamilifu. Dhamana hii fungamanishi, inapaswa kujikita kuanzia ndani ya familia za
kikristo, kwenye Jumuiya ndogo ndogo, vyama vya kitume na Kanisa katika ujumla wake.
Katika
Ibada hii ya Misa Takatifu Watoto wa Utoto Mtakatifu kutoka katika Parokia kumi na
moja zinazounda Jimbo kuu la Nairobi, walijumuika kusali kwa pamoja, kwenye Parokia
ya Bikira Maria Malkia wa Amani, iliyoko Kusini mwa Nairobi. Kardinali Njue anawataka
viongozi wa Kanisa kutumia Ibada mbali mbali za Kanisa kwa ajili ya kuimarisha Imani
yao.
Kwa namna ya pekee, anawaalika Makleri, Watawa, Makatekista na Wazazi
kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni chumvi na mwanga wa Imani kwa wote wanaowahudumia.
Wajitahidi kuhakikisha kwamba, watoto wanapewa kipaumbele cha pekee kama sehemu ya
mchakato wa kurithisha imani ya Kristo na Kanisa lake kwa watoto hawa ambao kimsingi
ni jeuri na tumaini la Kanisa imara na thabiti kwa sasa na kwa siku za usoni.