"Majembe" ya Uongozi wa Shirika la Masista wa Ivrea yakamilika!
Shirika la Masista wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili la Ivrea, hivi karibuni
lilihitimisha maadhimisho ya mkutano wake wa thelathini na tano kwa kumchagua kwa
mara nyingine tena Mheshimiwa Sr. Palma Porro, kuwa Mama Mkuu wa Shirika kwa kipindi
kingine cha miaka sita.
Kabla ya kuchaguliwa
kwa mara ya kwanza kuliongoza Shirika, Sista Palma Porro alikuwa anafanya utume wake
nchini Tanzania kama mmissionari na mlezi wa Wanovisi, katika nyumba yao ya Malezi
iliyoko Miyuji, Jimbo Katoliki la Dodoma.
Katika utume wake wa kuliongoza Shirika,
atashirikiana kwa karibu zaidi na Washauri wake wakuu kama ifuatavyo: Sr. Anna Mastropasqua;
Sr. Salome Aoko Odongo, kutoka Kenya, ambaye pia amechaguliwa kwa mara ya pili katika
nafasi hii. Wengine ni Sr. Donatela Gareffa pamoja na Sr. Franca Pavin.
Shirika
la Masista wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili la Ivrea, linafanya utume wake
sehemu mbali mbali duniani. Barani Afrika wamejikita zaidi nchini Libya, Kenya na
Tanzania.
Mheshimiwa Sr. Palma Porro, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Ivrea,
katika barua yake kwa Masista wenzake, anawaalika kwa namna ya pekee wawe ni chumvi
ya dunia na mwanga wa mataifa, kauli mbiu ambayo iliongoza maadhimisho ya Mkutano
mkuu wa thelathini na tano wa Shirika.
Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa
na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita hivi karibuni, ni mwaliko kwa Watawa wa
Ivrea kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kujitahidi kumfahamu zaidi Yesu Kristo, ili
kuboresha uhusiano wa kibinadamu kwa kujikita zaidi katika mchakato wa mshikamano
na udugu.
Masista wa Ivrea wanatambua umuhimu wa Imani kama nguvu inayoleta
mabadiliko ya ndani kwa kuwa makini katika mustakabali wa maisha yao kwa siku za usoni,
ukweli wa wito wao katika historia, maana ya maisha na kwamba, wao ni wasafiri kuelekea
Yerusalemu ya mbinguni.
Mheshimiwa Sr. Palma anasema kwamba, mara baada ya
maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Shirika, Masista wameendelea kusali na kusubiri kwa
hamu ili kufahamu majina ya wale waliopewa dhamana ya kuliongoza Shirika katika Kanda
mbali mbali.
Ni kipindi ambacho wamekuwa wazi kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu,
wakafanya hija ya Imani, kwa kutambua changamoto na fursa mbali mbali zilizoko mbele
ya Shirika na hatimaye, kuchagua watu ambao watawasaidia watawa wenzao kuendelea na
hija ya uaminifu kwa wito wao wa kitawa, karama ya Shirika, lakini zaidi kwa kuwa
ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.
Anawashukuru kwa namna ya pekee, Masista
waliokuwa wamepewa dhamana ya kuliongoza Shirika kwenye Kanda mbali mbali, kwa mfano
Mheshimiwa Sr. Raffaela Franzin aliyekuwa Mama Mkuu wa Kanda ya Malaika Mkuu Mikaeli,
inayowaunganisha Masista wa Ivrea wanaotekeleza utume wao Barani Afrika.
Shirika
limemchagua Mheshimiwa Sr. Enrica Agostina Giani kuwa Mama mkuu wa Kanda ya Malaika
Mkuu Mikaeli. Wengine waliochaguliwa ni pamoja na: Sr. Jenipher Muga atakayekuwa
Mama mkuu msaidizi wa Kanda. Sr. Assunta Malamso, Mshauri na Katibu wa Kanda. Sr.
Rosalia Henry, Mshauri. Sr. Adolfina Wambua, Mshauri Na Sr. Maria Rosaria Balestrucci,
Mweka hazina wa Kanda.
Mheshimiwa Sr. Enrica Agostina Giani na Washauri wake
wanatarajiwa kusimikwa rasmi hapo tarehe 16 Desemba 2012, Veyula, Jimboni Dodoma,
Tanzania. Tukio ambalo litasimamiwa na na Mheshimiwa Sr. Salome Aoko, Mshauri wa Shirika,
kutoka Makao Makuu, Roma.