2012-11-21 15:44:31

Fungueni akili zenu kwa mwanga wa ukweli wa Mungu unaoonesha utukufu wa utu na wito wa mwanadamu


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wakati wa Katekesi yake, Jumatano 21 Novemba, 2012, ameendelea kuwahimiza waamini kutambua maana ya imani, kama njia ya kukutana na mng'ao wa ukweli wa Mungu.

Kwa njia ya imani, mwamini anapata ufahamu kumhusu Mungu, yeye mwenyewe na kujifunza kuishi kwa busara katika ulimwengu huku akingojea utimilifu wa maisha na furaha ya uzima wa milele ujao. Imani na akili anasema Baba Mtakatifu ni mambo yanayofanya kazi kwa pamoja ili kufungua akili ya mwanadamu kuhusu ukweli wa Mungu. Kwa asili imani inapania kuelewa, wakati ambapo akili inatafuta ukweli, mwongozo na utimilifu wake kwa njia ya kukutana na Neno la Mungu ambalo limefunuliwa kwake.

Baba Mtakatifu anakazia kwamba, kimsingi hakuna msigano kati ya imani na sayansi, kwani yote yanapania kumhudumia mwanadamu katika maisha yake ya kimaadili na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji. Habari Njema ya Wokovu kuhusu Yesu Mwana wa Mungu, inaonesha ubinadamu ambao ni muhimu sana katika kulielewa Fumbo la Mwanadamu na Ulimwengu. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yawawezeshe waamini kufungua akili zao kwa mwanga wa ukweli wa Mungu, unaoonesha utukufu wa utu na wito wa mwanadamu.

Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa ushirikiano kati ya waamini wa Kanisa Katoliki na waaminiwa dini ya Kiislam, katika mchakato unaopania kudumisha haki katika ulimwengu mamboleo. Amewashukuru wanachama wa Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, CAFOD linaloadhimisha Jubilee ya miaka hamsini tangu lililopoanzishwa, kielelezo cha mshikamano wa upendo na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu anasema, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Novemba, iwe ni kielelezo na mfano wa kuigwa kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu sanjari na kutekeleza mapenzi yake. Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Watawa wa ndani, walioitwa kumfuasa Kristo kwa njia ya taamuli. Anapenda kuwahakikishia uwepo wake na ule wa Kanisa zima.

Anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwuwa, wanawasaidia watawa wa ndani kwa hali na mali, kwani wao ni msaada mkubwa kwani wamewekwa wakfu kwa ajili ya kuliombea Kanisa na Ulimwengu kwa ujumla.

Kumbu kumbu ya kutabarukiwa kwa Makanisa makuu ya Mtakatifu Petro na Paulo yaliyoko hapa mjini Roma, hivi karibuni, iwe ni chachu ya kukuza na kuimarisha upendo wao kwa Kanisa lililojengwa juu ya msingi wa maisha ya Mitume.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amewakumbusha waamini kwamba, Jumapili ijayo, Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, mwaliko kwa waamini kumweka Kristo kuwa ni kiini cha maisha yao, ili waweze kujichotea mwanga na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha ya kila siku.

Kwa wagonjwa na wote wanaoteseka, Msalaba wa Kristo uwe ni faraja na kielelezo cha mshikamano wa dhati na wanandoa wapya wanahimizwa kutambua uwepo wa Kristo kati yao na wanapoendelea na hija ya maisha ya ndoa, katika mchakato mzima wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika upendo na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.