Chama cha waamini walei wa Don Orione chatambuliwa rasmi
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, tarehe 20 Novemba 2012
limeandika Hati inayotambua Chama cha Waamini Walei wa Don Orione, kuwa ni kati ya
vyama vya walei vinavyotambuliwa rasmi na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.
Hili ni tukio ambalo linendelea kuongeza furaha na matumaini kwa Shirika la
Mabinti wa Neema ya Mungu, lililopitishwa na Vatican kunako tarehe 20 Novemba 1954.
Ilikuwa ni tarehe 6 Machi 1965 Shirika la Masista Wadogo wa Huruma lilipoidhinishwa
na tarahee 13 Mei 1997 Shirika la kitume la Orionino lilipitishwa pia.
Tukio
hili la kihistoria limeshuhudiwa na Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume pamoja na Mheshimiwa Padre Flavio
Peloso, Mkuu wa Shirika la Kazi za Don Orione pamoja na wakuu wengine wa Chama cha
Waamini Walei wa Don Orione.
Kikatiba sasa waamini hawa wataweza kushiriki
karama na tasaufi ya Shirika la Don Orione kikatiba baada ya kutambuliwa rasmi na
Mama Kanisa. Hili ni kundi ambalo limekuwa likiandamana bega kwa bega na Wamissionari
wa Don Orione katika maisha na utume wao na kwamba, wao ni matunda ya maadhimisho
baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Ilikuwa ni Mwaka 1992, takribani
miaka ishirini iliyopita, wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika, Chama
cha Waamini Walei wa Don Orione walipowaomba wajumbe kutunga Katiba pamoja na kuanza
mchakato wa kuratibu shughuli za Chama hiki na matunda ya jitihada hizi kwa sasa yameanza
kuonekana, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Chama hiki kimeenea
katika nchi thelathini, changamoto ya kuendelea kukikuza kwa kuwashirikisha walei,
watawa na makleri katika maisha na utume wao.