2012-11-20 09:05:09

Utume wa bahari na changamoto zake!


Kongamano la ishirini na saba kimataifa juu ya Utume wa Bahari, linaendelea kujadili kuhusu mchakato wa maboresho ya maisha ya mabaharia kwa kuwahakikishia huduma bora pamoja na kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho.

Haya ni kati ya malengo yanayofanyiwa kazi na Utume wa Bahari, kwa kuungana na Shirikisho la Wasafirishaji Kimataifa linalounganisha vyama vya wafanyakazi mia saba na nane, ili kuwawakilisha wafanyakazi zaidi ya millioni tano, wanaohudumia takribani nusu ya usafiri wa bahari duniani.

Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, wakiongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa mabaharia: nyenzo na mbinu mpya za kutangaza Habari Njema ya Wokovu." Wajumbe wanaendelea kutoa ushuhuda wa maisha yao binafsi jinsi ambavyo wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kuwwahudumia mabaharia sehemu mbali mbali za dunia.

Utume wa Bahari unawashirikisha watu wa dini na madhehebu mbali mbali, wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa mabaharia, kama ilivyojionesha kwa Mama Apinya Tajit, anayetekeleza utume wake kwenye Bandari za Thailand. Yeye anasema, anakutana zaidi na waamini wa dini ya Kiislam ambao wanafanya kazi baharini.

Kundi kubwa la mabaharia hawa wanajikuta wakati mwingine hawana chakula, wananyanyasika na kudhulumiwa haki zao msingi; wanatekwa na wakati mwingine wanakumbana na uharamia ambao kwa sasa umekuwa ni tishio kubwa katika usafiri wa bahari. Wao wanatoa huduma ya ushauri nasaha pamoja na kuhakikisha kwamba, walau wanapata mahitaji yao msingi kwa wakati huo.

Mradi wa ustawi wa jamii kwa ajili ya mabaharia nchini Italia, ni ushuhuda unaonesha kwamba, bandari zinaweza kugeuzwa kuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha urafiki na mahusiano mema. Kutokana na sababu za kiusalama, mabaharia wanapotua nanga hawaruhusiwi kushuka katika Meli zao kwa muda mrefu kutokana na hofu kwamba, wanaweza kutelekeza Meli zao na kuishia mitaani kutokana na sababu mbali mbali wanazokabiliana nazo.

Imetokea pia kwamba, kuna Meli zimeachwa bandarini na mabaharia kukosa mshahara, chakula na maji, kiasi hata cha kushindwa kurudi nyumbani kwao! Mtandao wa Utume wa Bahari umekuwa mstari wa mbele kuwasaidia Mabaharia hawa katika shida na mahangaiko yao, jambo ambalo kwa hakika, limejenga utamaduni wa upendo na mshikamano.

Kimsingi, mabaharia wanakabiliana na hali ngumu ya maisha wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, lengo la Utume wa Bahari ni kushiriki katika maboresho ya maisha ya wafanyakazi hawa, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi; huku wakikazia ubora wa vyombo vinavyotumika.

Tarehe 21 Novemba 2012, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wavuvi Duniani, fursa nzuri kwa ajili ya kuwakumbuka wavuvi kutokana na changamoto zinazowasibu katika maisha yao! Hatari na mazingira magumu wanayokumbana nayo, ili kuhakikisha kwamba, walau watu wengi wanapata kitoweo cha samaki mezani. Ni kundi linalo nyanyasika na kudhulimiwa, linalohitaji kutetewa kadiri ya sheria za kimataifa, ili hatimaye, kukidhi mahitaji ya mabaharia sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.