Mmeimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, sasa mnatumwa ulimwenguni ili kumshuhudia
Kristo na Kanisa lake kwa ujasiri mkubwa zaid!
Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, mapema juma hili ametembelea Parokia
ya Bikira Maria Malkia wa Damu Azizi ya Yesu, Kisasa na kutoa Sakramenti ya Kipaimara
kwa Wakristo sabini wa Kigango cha Mtakatifu Anna.
Katika mahubiri yake, Askofu
Nyaisonga anawataka Wakristo wote kutambua dhamana na jukumu lao katika maisha na
utume wa Kanisa, kwani wanahamasishwa kujikita katika umoja na mshikamano, furaha
na upendo mkamilifu; daima wakijitahidi kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake, kwa njia ya kuwatangazia wengine Habari Njema ya Wokovu, inayojikita
katika maisha yao ya kila siku.
Shida na magumu ni sehemu ya mchakato wa hija
ya maisha ya mwanadamu, lakini mambo haya yasiwafanye waamini kushindwa kuishi kwa
furaha na matumaini. Wanahimizwa na Kanisa kuwa kweli ni wajenzi wa misingi ya haki,
amani na umoja wa kitaifa, daima wakijitahidi kutafuta mafao ya wengi. Mifano bora
ya maisha, ni shule tosha kabisa ya utakatifu, unaoweza kuwasaidia wengine kuepuka
fursa za dhambi, daima wakijitahidi kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu.
Askofu
Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, ametoa sakramenti ya Kipaimara kwa Wakristo
sabini, ambao kwa sasa wanakuwa ni Mabalozi wa Kristo, tayari kumshuhudia kwa ujasiri
mkubwa, hata kiasi cha kuyamimina maisha yao. Wameimarishwa na Mapaji ya Roho Mtakatifu,
yawawezeshe kuadhimisha vyema Mwaka wa Imani, wakijitahidi pia kuendelea kuiboresha
Imani hii, kwa njia ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti pamoja na matendo ya
huruma.