Kitabu kuhusu Simulizi za Utoto wa Yesu chazinduliwa!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amezindua kitabu chake kuhusu simulizi za
Utoto wa Yesu wa Nazareti na wakati wowote kuanzia sasa, kitabu hiki kitaanza kuuzwa
madukani. Kitabu kimekwisha tafsiriwa katika lugha tisa za kimataifa; kati ya hizo
kuna: Kiitaliani, Kiingereza, Kifaransa, Kireno, Kihispania, Kijerumani na Kipolandi.
Kitabu hiki kimechapishwa katika nchi hamsini na tayari kimekwisha vuka nakala millioni
moja.
Taarifa zinabainisha kwamba, katika siku za hivi karibuni, kitabu hiki
kitaweza kuchapishwa katika nchi sabini na mbili katika lugha ishirini. Kitabu kimezinduliwa
na Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Hiki ni kitabu
kinachouliza swali la msingi, Je, ni kweli juu ya simulizi zilizoandikwa? Yesu ni
nani? NI swali ambalo Yesu mwenyewe aliwahi kuwauliza wafuasi wake kama inavyosimuliwa
kwenye Injili ya Marko, lakini ninyi mnasema kuwa mimi ni nani?
Maswali haya
msingi yanajibiwa kwa ufasaha kabisa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
katika kumfahamu Yesu wa Nazareti, kitabu ambacho kina kurasa mia moja na sabini na
sita, kimegawanyika katika sura nne, zikiwa na utangulizi mfupi na hitimisho lake.
Sura ya kwanza inazungumzia kuhusu ukoo wa Mkombozi kadiri ya Injili ya Mathayo na
Luka, wanaotofautiana, lakini wanamwingiza Yesu katika historia na uwepo wake kama
mwanzo mpya wa historia ya ulimwengu.
Sura ya pili, inajikita katika tangazo
la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji na Yesu. Baba Mtakatifu anasoma kwa mara nyingine
tena mahojiano kati ya Bikira Maria na Malaika Gabrieli, mintarafu Injili ya Luka
na kwa njia ya Bikira Maria, mwenyezi Mungu anatengeneza njia mpya ya kuingia duniani,
ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti, ili kutekeleza dhamana hii,
Mwenyezi Mungu anahitaji utii mkamilifu unaojikita katika uhuru wa kutimiza mapenzi
ya Mungu. Kwa namna moja, Mwenyezi Mungu anaamua kumtegemea mwanadamu na nguvu yake
inategemea jibu la "Ndiyo" ili kuanza historia ya ukombozi.
Sura ya tatu, inaonesha
tukio la kuzaliwa kwa Yesu wa Nazareti mjini Bethlehemu; kwa kuwataja wahusika wakuu,
wanaomwezesha kuiweka historia hii katika uwanja mpana zaidi wa kimataifa, ili kumkirimia
mwanadamu ukombozi kama kielele cha utimilifu wa nyakati. Kila jambo linalosimuliwa
hapa lina utajiri mkubwa kuhusu maisha ya Yesu anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita.
Mwana mpendwa wa Mungu anazaliwa katika hali ya umaskini, kielelezo
cha mshikamano wa Mungu na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii,
wanaowakilishwa na wachungaji wanaosikia wimbo wa utukufu wa Mungu ukiimbwa. Baba
Mtakatifu anasema, hapa kuna kinzani katika kufasiri maneno yaliyoko kwenye wimbo
wa "Utukufu kwa Mungu juu".
Mamajusi na wataalam wa nyota waliiona nyota yake
Mashariki, wakaja kumsujudia Mfalme wa Wayahudi pamoja na kukimbilia uhamishoni Misri
ni utajiri mkubwa wa simulizi juu ya Utoto wa Yesu wa Nazareti unaopatikana kwenye
Sura ya Nne ya Kitabu cha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Mamajusi hawa
wanaelezewa kwa kina kwa kuzingatia misingi ya kihistoria na kisayansi, ni watu wanaotafuta
kuzima ile kiu ya ndani ya maisha ya mwanadamu.
Baba Mtakatifu anahitimisha
kitabu chake kwa kufanya rejea kadiri ya Simulizi za Mwinjili Luka kuhusu Utoto wa
Yesu, matukio machache kabisa kabla ya kuanza utume wake hadharani kwa Ubatizo Mtoni
Yordani. Tukio la siku tatu, kabla ya kuanza hija ya maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka,
pale Yesu alipoamua kubaki nyuma na kuwaacha wazazi wake; Bikira Maria na Yosefu,
akaa Hekaluni kwa muda wa siku tatu akijadiliana na Walimu wa sheria. Yesu akazidi
kuendelea kukua katika hekima, kimo na neema. Hii ni sehemu inayomwonesha Yesu kuwa
ni Mungu kweli na mtu kweli, aliyefikiri na kujifunza katika mtindo wa kibinadamu.
Itakumbukwa kwamba, vitabu viwili vilivyotangulia, Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, ameandika kuhusu: Maisha ya Yesu Hadharani, tangu alipobatizwa hadi
alipogeuka sura na kitabu cha pili ni kuhusu Yesu alipoingia kwa shangwe Yerusalem
hadi Ufufuko. Ni vitabu ambavyo vimechapishwa kunako mwaka 2007 na mwaka 2011.