Yesu Kristo ni mwamba wa matumaini thabiti, kamwe hauwezi kuyumba!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili
tarehe 18 Novemba 2012, alitafakari kuhusu sehemu ya Injili ya Marko, inayogusia kwa
namna ya pekee, mambo ya nyakati za mwisho; yaani: kifo, hukumu, Paradiso na uzima
wa milele. Hii pengine ni kati ya sehemu ngumu sana kueleweka kwenye Injili ya Marko,
kutokana la ugumu wa yaliyomo na lugha inayotumika.
Ni sehemu ya Injili inayozungumzia
mambo yanayozidi ufahamu wa akili ya mwanadamu, jambo linalomfanya Yesu kutumia mifano
na maneno kutoka katika Agano la Kale, lakini anakazia kwamba, Yeye mwenyewe ni kiini
cha Fumbo hili kutokana na mateso, kifo na ufufuko wake. Injili ya Marko, Jumapili
ya thelathini na tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, anasema Baba Mtakatifu inaonekana
kuwa na vitisho, lakini ujumbe unapatikana ile sehemu ya mwisho, watakapomwona Mwana
wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.
Yesu mwenyewe anaunganisha
historia iliyopita, iliyoko na ile ijayo na kwamba, ni utimilifu wa utabiri uliotolewa
na Manabii katika Agano la Kale. Licha vurugu na vitisho vitakavyojitokeza, lakini
Yesu anabakia kuwa ni Mwamba thabiti na kamwe hawezi kutikisika! Huu ndio ujumbe wa
Injili, Jumapili ya thelathini na tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, anasema Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Neno la Mungu ni kiini cha kazi ya uumbaji na
viumbe vyote vinapaswa kuliheshimu Neno la Mungu.
Nguvu ya Uumbaji kutoka katika
Neno la Mungu inajikita zaidi kwa Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, nguvu
inayoongoza mawazo na maneno ya binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.
Yesu anapenda kuwasaidia wafuasi wake kuifahamu ile Siku ya Mwisho, kwa kuondokana
na wasi wasi unaojikita katika tarehe na utabiri, anawaonesha njia mwanana wanayopaswa
kuitumia ili kufikia maisha ya uzima wa milele. Yesu anasema kwamba, kila kitu kitapita,
lakini Neno la Mungu kamwe halitapita na kwamba, kila mtu atahukumiwa kutokana na
matendo yake.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anabainisha kwamba,
hata nyakati hizi kuna maafa asilia, vita na kinzani mbali mbali. Dunia inahitaji
kuwa na Mwamba wa matumaini thabiti ili watu wasitumbukie katika mawazo mepesi mepesi.
Anamwomba Bikira Maria awasaidie waamini na watu wenye mapenzi mema, kumpokea Kristo
kwa njia ya Neno lake. Anawaalika waamini kuwa waaminifu kwa Mungu na Kanisa, kwa
kushiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu.