2012-11-19 15:13:14

Viongozi wa kidini Tanzania dumisheni: haki, amani, umoja na mshikamano; chokochoko za kidini ni hatari!


Askofu mkuu Alex Malasusa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania, Jumapili iliyopita amemsimika Mchungaji Amon Kinyunyu kuwa Askofu wa Dayosisi ya Dodoma na kuwataka viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kuimarisha amani kwani hili ni jina jipya la maendeleo ya watu duniani. Pasi amani, Tanzania itadumaa katika mikakati yote ya maendeleo inayopangwa kwa sasa.

Wananchi wanapaswa kutumia vyema uhuru wao wa kuabudu, bila kuhatarisha amani na usalama wa wananchi wengine nchini Tanzania. Matumizi ya mabomu ya machozi ni dalili mbaya kwa amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania, kwani kinachofuata ni matumizi ya risasi za moto, jambo litakalogumisha hata masuala ya Ibada mbali mbali.

Viongozi wajitahidi kuonesha dira na mwanga wa kufuata na katika maisha yao ya kiroho, daima wakijitahidi pia kuwasaidia ili kujikomboa: kiuchumi na kijamii, kwani mwanadamu ameumbwa mwili na roho.

Kwa upande wake, Askofu Amoni Kinyunyu, amewataka waamini wa Kanisa la Kiijili la Kiluteri Tanzania, Dayosisi ya Dodoma kuenzi shughuli mbali mbali zilizofanywa na Askofu mtangulizi wake katika maendeleo ya roho na mwili Jimboni hapo. Askofu mstaafu Festo Ngowo atakumbukwa sana kutokana na mikakati ya ujenzi wa Sekondari, ujenzi wa Ofisi za Dayosisi hiyo pamoja na miradi inayopania kumkomboa mwamini: kiroho na kimwili. Askofu Ngowo amelazimika kung'atuka madarakani baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi, amewataka viongozi wa dini kuhubiri na kusimamia misingi ya haki, amani na utulivu na kamwe wasijiingize katika kuchochea vurugu miongoni mwa Jamii. Watanzania watumie uhuru wa kuabudu uliotolewa na Serikali kwa kuheshimu na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Chokochoko za kidini ni hatari kwa mustakabali wa Taifa. Viongozi wanapaswa kuwa ni wachamungu na vikolezo vya maendeleo, haki, amani, maadili na utu wema.







All the contents on this site are copyrighted ©.