2012-11-19 09:24:39

Ujumbe wa matashi mema kwa Papa Tawadros II anapoanza kutekeleza utume wake!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemtumia ujumbe wa matashi mema Papa Tawadros II, Patriaki wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox, baada ya kusimikwa rasmi kuwa Papa wa Alexandria na Patriaki wa Kanisa kuu la Mtakatifu Marko.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha Umoja wa Wakristo, ambaye amemhakikishia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa njia ya sala na sadaka yake takatifu, wakati huu anapoanza kutekeleza utume wake kama Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodox.

Anamwombea wingi wa neema na baraka anapowaongoza waamini wake katika hija ya utakatifu wa maisha; anawatakia amani na maendeleo. Baba Mtakatifu anakumbuka wema na ukarimu wa mtangulizi wake Papa Shenouda wa tatu, aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Watu wa Mungu aliokuwa amekabidhiwa kwake. Alijitahidi kuboresha mahusiano na Kanisa Katoliki, ili siku moja, Wakristo waweze kuwa wamoja katika upendo na upatanisho chini ya Kristo mwenyewe.

Baba Mtakatifu anamwombea mapaji ya Roho Mtakatifu anapotekeleza utume wake, ili waonje kwa hakika mafundisho ya Mchungaji Mwema; wakiwa na utulivu wa ndani, daima wakijitahidi kushiriki katika ujenzi wa Jamii inayowazunguka na kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anaombea pia uhusiano kati ya Makanisa haya mawili uendelee kuboreka, katika moyo wa ushirikiano wa kidugu sanjari na tafakari ya kina ya taalimungu, ili kujenga umoja na hatimaye, kutoa ushuhuda mbele ya ulimwengu kuhusu Kweli za Kiinjili zinazookoa.







All the contents on this site are copyrighted ©.