2012-11-19 14:41:02

Rais Thomas Boni Yayi wa Benin akutana na Baba Mtakatifu mjini Vatican


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu, tarehe 19 Novemba 2012 amekutana na kuzungumza na Rais Thomas Boni Yayi na ujumbe wake na baadaye kukutana pia na ujumbe wa Vatican uliokuwa unaongozwa na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.

Viongozi wa pande hizi mbili wamezungumzia kwa kina na mapana uhusiano mwema uliopo kati ya Benin na Vatican. Wamefanya rejea ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita nchini Benin wakati wa kuzindua matunda ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, Novemba 2011. Wamegusia pia mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha maendeleo ya nchi ya Benin.

Kwa namna ya pekee, viongozi hawa wawili wamejadili kwa mapana kidogo kuhusu utamaduni wa wananchi wa Benin na Afrika kwa ujumla wake; umuhimu na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu; katika mchakato wa kudumisha haki, amani na upatanisho wa kweli.

Wamejadili pia changamoto zinazolikabili Bara la Afrika kwa wakati huu, kutokana na dhamana aliyo nayo kwa sasa Rais Thomas Boni Yayi ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.