2012-11-19 07:47:45

Kazi isaidie kudumisha na kuimarisha uhusiano ndani ya Familia na Jamii


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika kipindi chetu kilichopita tulikazia kuwa kazi ni wito au mwaliko aliopewa mwanadamu na Mungu mwenyewe katika uumbaji. RealAudioMP3
Leo nakualika tuangalie jinsi kazi ilivyo na uhusiano mkubwa na maisha ya jumuiya. Kazi lazima iimarishe mahusiano na Mungu, binadamu pamoja na viumbe vingine.
Kazi ambayo mwanadamu anaifanya kuyawesheza maisha yake ambayo pia ni kipimo cha utu wake ina chimbuko na kilele chake katika mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu na kati ya mwanadamu na mwanadamu mwingine.
Ni bahati mbaya leo kuwa mfumo wa kiuchumi na ushindani wa uzalishaji umeendelea kuweka mtengano mkubwa kati ya uchumi na mahusiano, kati ya kazi na upendo. Hapa ni vizuri tutaje tena kuwa endapo kazi itawageuza watu kuwa mashine za uzalishaji tu bila mahusiano mazuri sio fikira sahihi.
Wakati wote ni lazima itambulike kuwa, kazi ina chimbuko na kilele chake katika familia. Mwenyeheri Papa Yohane Paulo II na hata Papa Benedikto XVI katika Mafundisho yao kuhusu jamii (social teachings) wanarudia kusema kazi na uchumi ni mali zenye dhamani za kijamii (social goods) zote zina chimbuko na kilele chake katika maisha ya familia na jamii.
Kwa huluka yake mwanadamu hawezi kufikirika nje ya jamii au nje ya mahusiano na Muumba wake. Ndio sababu hata wahenga wetu wanakiri kuwa hakuna mwanadamu aliye tajiri wakutohitaji msaada wa mwingine lakini pia hakuna masikini wa kutoweza kuchangia lolote katika maisha.
Tusichoke tena kurejea katika utamaduni wetu mzuri wa Kiafrika ambapo hakuna tukio la mtu binafsi ila kila tukio lilikuwa mali ya jumuiya lilitendwa au kuwagusa wanajamii wote. Kati maana hii kweli kazi isaidie kuimarisha mahusiano ya kijumuiya na isiwe sababu ya utengano kwani kila mmoja ana mchango wake ambao hauwezi kubebwa na mwingine.
Kazi ambayo mwanadamu anajikuta kwayo tangu siku ya kwanza ya uwepo wake inadai mahusiano na muumba wake kwani ni wito anaoupokea toka kwake. Katika maana hii mwanadamu lazima afanye kazi kulingana na matakwa ya muumba wake na sio kwa matakwa yake. Lakini hata hivyo mwanadamu hapewi utume huu katika ubinafsi wake bali katika mahusiano na mwanadamu mwingine na pia na viumbe vingine. Ni katika kazi mwanadamu ana upa hadhi ubinadamu wake uliofanyizwa kwa sura na mfano wa Mungu mwenyewe.
Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphael Mwanga, wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo kikuu cha kipapa Laterano- Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.