Kanisa Katoliki nchini Nigeria linazidi kukua na kupanuka, matendo makuu ya Mungu!
Askofu mkuu John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria ni kati ya Makardinali
wateule watakaosimikwa rasmi Jumamosi ijayo hapa mjini Vatican na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita. Kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu ni ishala ya kukua na
kukomaa kwa Kanisa Katoliki nchini Nigeria, licha ya kinzani na changamoto mbali mbali
zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.
Tukio la kusimikwa
kwake kuwa Kardinali, linatarajiwa kuhudhuriwa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi
mema zaidi ya mia mbili kutoka Nigeria, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Padre Patrick
Tor Alumuku, mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano, Jimbo kuu la Abuja, Nigeria.
Tangu
kuteuliwa kwake, Kardinali mteule Onaiyekan ameendelea kupokea ujumbe wa pongezi na
matashi mema kutoka kwa viongozi wakuu wan chi na Kanisa ndani na nje ya Nigeria.
Waamini wanaendelea kumshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hata kwa
kumteua Monsinyo Fortunatus Nwachukwu, kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini
Nicaragua. Zote hizi ni dalili za kukua na kukomaa kwa Kanisa Katoliki nchini Nigeria,
kiasi kwamba, linaweza kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu.
Kuna idadi kubwa ya waamini nchini Nigeria na kwamba, miito inazidi kuongezeka siku
hadi siku.
Kanisa nchini Nigeria ni mhimili mkuu wa maendeleo ya watu: kiroho
na kimwili; dhamana inayojionesha kwa namna ya pekee kabisa katika utoaji wa huduma
kwenye sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya wananchi wa Nigeria. Kwa sasa
Kanisa linaendelea kuwekeza katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, ili
kuweza kufikisha ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa watu wengi zaidi, ikilinganishwa
na hali ya sasa.