Askofu mkuu Guido Pozzo awekwa wakfu: kielelezo cha huduma ya upendo wa Khalifa wa
Mtakatifu Petro kwa wahitaji zaidi
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, mwishoni mwa juma, amemweka wakfu
Monsinyo Guido Pozzo, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
wa kumi na sita kuwa Mhudumu mkuu wa Sadaka ya Papa, kuwa Askofu mkuu.
Ibada hii
imefanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Lorenzo in Damaso. Ni mtu ambaye Baba Mtakatifu
anamfahamu fika, kwani walikwishawahi kufanya kazi kwa pamoja katika Baraza la Mafundisho
Sadikifu ya Kanisa na sasa kwa kuwekwa wakfu anakuwa ni sehemu ya Familia ya Khalifa
wa Mtakatifu Petro.
Katika mahubiri yake, Kardinali Bertone anasema kwamba,
furaha ya kweli inapatikana kwa kujitoa bila ya kujibakiza katika utoaji wa huduma
makini, hasa pale anapoadhimisha na kuwagawia waamini Mafumbo ya Kanisa; hapa inakuwa
kweli ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka katika Imani kwa Kristo na Kanisa
lake. Furaha hii ioneshe moyo wa mshikamano, utambulisho wa kuwa Mkristo na Imani
ya kweli. Ni mwaliko wa kuwagawia wengine, imani, matumaini na mapendo.
Kwa
kuwekwa kwake wakfu kuwa Askofu mkuu, jina lake linaandkiwa katika kitabu cha waandamizi
wa mitume, wale ambao kwa njia ya Roho Mtakatifu wanaendeleza Kanisa la Mungu, kama
wachungaji na walimu wa Kanisa.
Kwa namna ya pekee, Kardinali Bertone anawaalika
waamini kuwa na imani na matumaini kwa Kristo na kamwe wasikubali kuelemewa na vitisho
vinavyosimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini na tatu
ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Watambue kwamba, Kristo atakuja tena kuwahukumu wazima
na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho, changamoto kwa wafuasi wa Kristo
kumwilisha ndani mwao Injili ya Upendo.
Mama Kanisa
anatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwashirikisha wote ule upendo unaibubujika
kutoka kwa Mwenyezi Mungu; upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa
na huduma bora kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waonje
joto la imani inayotolewa ushuhuda wa kweli katika mshikamano wa upendo.Waamini wanachangamotishwa
kutolea ushuhuda wa imani yao kwa ari na moyo mkuu. Huu ndio utume ambao Askofu mkuu
Guido Pozzo anaalikwa kuutekeleza kwa niaba ya huduma ya upendo inayotolewa na Khalifa
wa Mtakatifu Petro.
Ni huduma ya upendo na mshikamano inayojikita katika maisha
ya kawaida kabisa na wakati mwingine katika hali ya ukimya kama kielelezo cha udugu
na mshikamano wa Kikristo, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, kwa maskini, wahitaji na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Huduma ya upendo ni utume wa kila mwamini anasema Kardinali Bertone, lakini
ni wajibu fungamanishi kwa viongozi wa Kanisa waliyopewa dhamana ya kuwaongoza, kuwafundisha
na kuwatakatifuza watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Ni wajibu wao kutekeleza dhamana
hii mintarafu dira na mwongozo wa Yesu Kristo mchungaji mwema.
Huduma ya upendo
inaunganisha utambulisho wa kitaalimungu na maisha ya kiroho yanayojionesha kwa namna
ya pekee kwa Askofu anapotekeleza utume wake katika shughuli za kichungaji. Ni mwaliko
wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa njia hii, Kristo
anaendelea kumhudumia mwanadamu.
Hii ndiyo changamoto endelevu atakayokabiliana
nayo Askofu mkuu Guido Pozzo wakati wa utekelezaji wa dhamana na utume wake kwa Kanisa.
Umefika wakati wa kudhihirisha yale majiundo makini aliyoyapata katika hatua mbali
mbali za maisha yake kama Padre na sasa kama Askofu; ni muda wa kuonesha upendo mkamilifu
kwa Kristo, Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuendelea kushuhudia utajiri wa
huduma aliyokuwa anaitoa kwa miaka mingi hapa Vatican, katika nyadhifa mbali mbali
alizokabidhiwa na Mama Kanisa.