Wahudumu wa sekta ya afya tangazeni Injili ya Upendo, Uhai na Matumaini kwa kuwa waaminifu,
makini na wenye huruma!
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa
wafanyakazi katika sekta ya afya, Jumamosi, tarehe 17 Novemba 2012 ameadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican kwa ajili ya washiriki
wa Kongamano la Madaktari Wakatoliki kutoka Ulaya uliokwenda sanjari na Mkutano wa
ishirini na saba wa afya kimataifa ulioandaliwa na Baraza lake.
Katika mahubiri
yake, Askofu mkuu Zimowski amewaalika wafanyakazi katika sekta ya afya kuendelea kuwa
waaminifu katika maisha na utume wao kwanza kabisa kwa Kristo na Kanisa; kwa wagonjwa
na wote wanaoteseka wakitambua kwamba, wao kimsingi wanaalikwa kuhudumia Injili ya
Uhai, kwani maisha ya mwanadamu ni matakatifu kwa sababu yanapata chimbuko lake kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Anawataka wawe wahudumu makini, daima wakiendelea kukesha
na kusoma alama za nyakati mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Watoe huduma kwa wagonjwa
huku wakisukumwa na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, daima wakijitahidi kutenda mema
na wala wasikatishwe tamaa katika huduma na maisha yao ya Kikristo.
Mambo makuu
matatu wanapaswa kuyazingatia nayo ni kukesha kwani hawajui siku wala saa atakapokuja
Mwana wa Mtu. Hiki kiwe ni kipindi cha kutekeleza mapenzi ya Mungu katika hija ya
maisha yao hapa duniani; ni mwaliko wa kuwasha taa ya imani inayomwilishwa kwa njia
ya upendo wa dhati; changamoto iliyofanyiwa kazi na watakatifu wengi ndani ya Kanisa.
Anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kumtafuta, kumpenda na kumhudumia Kristo
kwa njia ya ndugu zake walio wadogo zaidi, wanaoelemewa na magonjwa, uzee, upweke
na wakati mwingine wanabaguliwa kutokana na hali yao ya maisha. Wote hawa waonjeshwe
Injili ya Upendo.
Wafanyakazi wa sekta ya afya, kimsingi ni watangazaji wa
Injili ya Uhai ambayo wanapaswa kuwaonjesha jirani zao kwa njia ya huduma makini,
ukweli na ushuhuda wa maisha yao, hasa katika ulimwengu mamboleo ambamo watu wengi
wanakabiliwa na ukavu wa maisha ya kiroho kutokana na kuelemewa na malimwengu; wote
hawa wanahitaji waamini wanaojifunga kibwebwe ili kushuhudia imani yao sanjari na
kuyatakatifuza malimwengu.
Ni changamoto ya kusimama kidete dhidi ya Utamaduni
wa kifo, kwa kutangaza kwa nguvu na ari kuu zaidi Utamaduni wa uhai, kwa kutambua
na kuenzi utambulisho wao unaopata chimbuko lake katika Ukristo.
Injili ya
Kristo iwe ni dira na mwongozo katika utekelezaji wa majukumu la taaluma yao, kwani
Injili ya Matumaini kamwe haiwezi kumdanganya mtu! Utume huu wanapaswa kuutekeleza
kwa ujasiri mkubwa Barani Ulaya kwa kutangaza Injili ya Matumaini kwa watu wanaokata
tamaa, lakini zaidi, kwa kuwahudumia wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii. Waimarishe Imani yao kwa njia ya ushiriki wao katika Fumbo la Ekaristi Takatifu,
wanamo tangaza: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kiini cha Imani ya Kanisa.
Utangazaji
wa Injili ya Matumaini ujioneshe hasa katika maeneo ya kazi kwa kulinda na kutetea:
maisha, utu na heshima ya mwanadamu; umoja na mshikamano kati ya watu, kwani wote
hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu: wawe ni vyombo vya upatanisho barani Ulaya,
vinavyomwelekea Yesu Kristo mkombozi wa ulimwengu.