Sayansi ya Kikristo juu ya mateso inafumbatwa katika: mguso, mshikamano, majitoleo
ya dhati na kushirikishana
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi tarehe17 Novemba 2012, aliwapongeza
wajumbe wa mkutano mkuu wa ishirini na saba wa afya kimataifa uliokuwa unaongozwa
na kauli mbiu "Hospitali, mahali pa Uinjilishaji: utu wa kiutu na kiroho; sanjari
na wajumbe wa kongamano la Shirikisho la Madaktari Wakatoliki Italia na Ulaya, waliokuwa
wanajadili kuhusu maadili ya kibayolojia na "Ulaya ya Kikristo", bila kusahau umati
mkubwa wa wagonjwa na wanafunzi wataalam katika sekta ya afya waliokuwa wanahudhuria
pia mikutano hii kama sehemu ya majiundo yao.
Baba Mtakatifu anasema, Kanisa
linawaangalia wagonjwa na wote wanaoteseka kwa moyo na upendo wa kidugu; likisukumwa
na roho ya Kristo ambaye kwa njia ya Fumbo la Mateso yake ameyapatia mahangaiko ya
mwanadamu utu na mwelekeo mpya, kwa kutambua kwamba, ni watu ambao si pweke na utu
wao una thamani kubwa, kwani, wanaunganisha mateso na mahangaiko yao katika Msalaba
wa Kristo, kama sehemu ya ushiriki wao katika mateso yanayookoa.
Kutokana na
mwaliko huu, Kanisa linapenda kuwawashia wataalam wa sekta ya afya na watu wanaojitolea
moyo wa matumaini, kwa kutambua kwamba, wana wito maalum kabisa, unaowawajibisha kujifunza
kwa bidii, juhudi na maarifa; kwa kuguswa na kutafuta mang'amuzi mapana zaidi. Wote
wanaojitosa kimasomaso katika wito huu, watambue kwamba wanashiriki utume wa maisha
ya kiutu na kiroho unaozidi hata vyeti vya taaluma walivyopokea.
Hii ni Sayansi
ya Kikristo juu ya Mateso, inayobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
kama ukweli pekee unaotoa jibu makini katika Fumbo la Mateso pamoja na kujitahidi
kuwahudumia kwa ufanisi mkubwa. Si wajibu wa Kanisa kuwapatia afya bora wala kuwapunguzia
mateso yao, lakini wanayo zawadi kubwa ambayo ni Kristo aliyeshiriki Fumbo la mateso
na mahangaiko ya binadamu, kielelezo cha ajabu kabisa cha thamani ya mateso ya mwanadamu.
Wafanyakazi katika sekta ya afya ni wataalam waliobobea katika Sayansi ya
Mateso ya Mwanadamu. Utambulisho wao wa Kikatoliki unawapatia wajibu na dhamana nyeti
sana ndani ya Jamii na Kanisa; huu ni wito wa pekee kabisa kama ambavyo wamedhihirisha
watakatifu kama vile: Giuseppe Moscati, Mtakatifu Ricardo Pampuri, Mtakatifu Gianna
Beretta Mola, Mtakatifu Anna Schaffer pamoja na Mtumishi wa Mungu Jèrome Lejeune.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema kwamba, wakati huu wa Uinjilishaji Mpya
na myumbo wa uchumi kimataifa, kuna haja ya kutafuta rasilimali zitakazoweza kusaidia
kulinda na kutetea afya; hospitali, vituo vya afya vinapaswa kuwa ni mahali pa kudumisha
mafao ya wengi na kamwe afya isifanywe kuwa ni bidhaa kwa ajili ya wateule wachache
ndani ya Jamii.
Utu n a heshima ya wagonjwa vilindwe na kudumishwa na kwamba,
maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba yasaidie kutoa tiba ya mtu mzima: kiroho
na kimwili; kwa kuzingatia kanuni, maadili na utu wema, kwani wito wa Madaktari ni
kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu katika kila hatua ya maisha yake hapa duniani.
Sayansi
ya Kikristo kuhusu mateso inajikita zaidi kwa mtu kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko
ya jirani zake; mshikamano, majitoleo, kushirikishana, ili hatimaye, kuwa ni walimu
wa kweli kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Maneno ya Msamaria mwema yawe ni msingi
thabiti katika kukuza na kudumisha utamaduni wa maadili na utu wema.
Kutokana
na mwelekeo kama huu, Hospitali inakuwa ni mahali pa Uinjilishaji, kwani ni mahali
hapa ambapo Kanisa linaonesha kwa namna ya pekee kabisa uwepo wa Mungu kwa kuthamini
na kujali utu na heshima ya binadamu. Kiini cha huduma zinazotolewa na sekta ya afya
ni binadamu katika hali zake zote, binadamu anayehitaji kulindwa na kushirikishwa
maana ya Fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu.
Mgonjwa aonje uhusiano
wa utume wa upendo anapokuwa Hospitalini, mahali ambapo upendo wa Msamaria mwema unajionesha
kwa namna ya pekee kabisa kwa kutambua pia kuwa sura ya mgonjwa ni sura ya Kristo.
Wafanyakazi katika sekta ya afya wanakabiliwa na utume wa kutoa tiba na kuinjilisha
kwa kutambua kwamba, ulimwengu mamboleo unahitaji sana Wasamaria wema, watu wenye
moyo wa ukarimu na wanaonyoosha mikono yao tayari kuwakumbatia wote, kwa kutambua
kwamba, huu ni wajibu ambao ni kipimo cha huduma yao kwa Jamii.
Ni huduma
kama hii inayopita uwezo wa mwanadamu, inayotekelezwa na Makleri na Watawa katika
sekta ya afya, ili kuhakikisha kwamba, Fumbo la Mateso ya mwanadamu linapata mwanga
kutoka kwa Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka.
Mwishoni, Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, anawaambia wagonjwa kwamba, ukimya wao ni ushuhuda makini
katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya, wale wanaowatibu na kuwahudumia kwa matumaini
kwamba, hakuna hata chozi la mtu awaye yote litakalopotea bure machoni pa Mwenyezi
Mungu.
Wagonjwa ni ndugu zake Kristo katika mateso yao na kwamba, kwa njia
ya mateso yao wanashiriki katika wokovu wa dunia. Baba Mtakatifu anawaweka wagonjwa
na wafanyakazi wote katika sekta afya chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria
afya ya wagonjwa, ili aweze kuongoza mapito yao, daima wakiwa ni mashahidi wa Sayansi
ya Kikristo kuhusu mateso.