Mikakati ya CUEA katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya Chuoni hapo!
Monsinyo Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki
na Kati, CUEA katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa Uinjilishaji
Mpya unaondeshwa CUEA kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliozinduliwa
hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.
Dhamana hii
inatekelezwa kwa namna ya pekee kwa njia ya utume wa maisha ya kiroho kwa wanafunzi
wa Chuo Kikuu pamoja na kuendelea kuimarisha vyama vya kitume ambavyo ni msaada mkubwa
katika maisha ya kiroho kwa wanafunzi.
CUEA inaendelea kujiimarisha ili kuhakikisha
kuwa inawajengea wanachuo wake uwezo wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia
Mungu na jirani sanjari na ujenzi wa misingi ya maadili na utu wema, changamoto endelevu
katika Jamii nyingi Barani Afrika. Mpango huu unakwenda sanjari na uwezeshwaji wa
viongozi wa Kanisa na kwa namna ya pekee, viongozi wa utume wa vijana, ili waweze
kutoa ushauri makini kwa vijana katika shida na mahangaiko yao ya ndani.