Kilele cha utamadunisho ni kushiriki katika utukufu wa Kristo!
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Padre Nikodemo Mayala katika makala haya amefafanua
vyema dhana nzima ya utamadunisho na kwamba, kilele cha utamadunisho ni kutaka kushiriki
utukufu wa Kristo, kwa kupata maisha ya uzima wa milele. Ninakusihi uendelee kujichotea
utajiri wa makala hii, ukiweza mshirikishe na jirani yako pia, kwani utamadunisho
ni dhamana endelevu katika hija ya maisha ya waamini. Tamaduni zinapokutana
hutokea nini? Mkutano, mawasiliano na mgusano wa tamaduni. Utamaduni wa kigeni
kukutana na utamaduni wa wakazi. Hatua hii muhimu hukanganya, maana mgeni huja na
chake, na mwenyeji analinda chake. Kila mmoja anathamini chake. Chake ni bora kuliko!
Mawasiliano ya awali ni mgongano na msuguano. Kukosa kuelewana, kupambana. Jitihada
ya wazi ni kujihami kwa kila namna. Ni hatua ya msingi kutafititi kutofautisha tamaduni
mbili katika msuguano. Wangu bora, wako bora!
Tutambue tamaduni zote si kamilifu.
Hivi mwingiliano ni wa lazima ili kutajirishana. Itakumbukwa kuwa alipofika mkoloni
na mlowezi, aliukoloni utamaduni, akaulowa utamaduni wa watu akapandikiza wa kikoloni.
Fahari ni kulonga kiingereza, kifaransa na kireno. Huu ndo uliitwa utamadunisho, ustaraabisho.
Aidha, Kanisa lilipopandikizwa, Kilatini ilikuwa kama lugha ya Mungu. Si lugha ya
mawasiliano kukutana na tamaduni za watu. Lakini Mungu katika nyakati zetu “amesema
na sisi katika Mwana” (Ebr.1:2).
Ikumbukwe kwamba, kwa sasa wale wote wanaopania
kuwa Mapadre, wanapaswa kuifahamu lugha ya Kilatini, kama anavyokazia Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, kumbe lugha ya Kilatini kwa Kanisa bado ina umuhimu wa
pekee.
Mlishizo. Hatua hii ni mithili ya kulishiza chakula baada ya mmeng’enyo
, kufanya mwenyeji; staarabika, staarabisha, similisha chukua, pata (maarifa, fikira,n.k.).
Tutakumbuka mlishizo, usimilishaji kuwa ilikuwa sera ya Wareno na Wafaransa katika
harakati zao kuwageuza wenyeji wafanane kama wao. Mlishizo Injili ni ustaarabishaji
wa wakazi kiinjili, kuwafanya wafanane na Kristo, si tena na mreno wala mfaransa.
Mapinduzi
ya kitamaduni: Mageuzoumbile, mabadilikoumbile. Hatua hii muhimu ya mabadiliko ni
ya makuzi. Tamaduni zinatajirishana, zinatakasana, na kila upande waafiki uongofu.
Mapokezi ya mageuzo na mbadiliko yanaunda utamaduni fungamanifu.
Twaweza kufananisha
mabadiliko umbile ya utamaduni na tukio la mng’aro wa Bwana wetu Yesu Kristo kule
mlimani kuwa ndo kilele cha utamadunisho.
Kutamadunisha twamanisha nini? Utamadunisho
kwetu ni wongofu. Watu wamwongekee Mungu. Utamadunisho ni kuruhusu Neno kukua na kukomaa
kwa kutumia virutubisho mahalia. Kwa maneno mengine utamadunisho wamanisha kuwa Ukristo
waweza kuota mizizi utakapotwaa mwili katika mifumo ya tamaduni. “Maana ilimpendeza
Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo ya lazima.”(Mdo.15:28).
Utamadunisho ni kukiri, kutambua utambulisho na tofauti. Mambo ya msingi ni wongofu
na ukamilifu. Mwanadamu atafute kumwongea Mungu ili apate ukamilifu katika Mungu.
Utamadunisho
wajumuisha: mawasiliano, tafsiri (toa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda nyingine
bila ya kubadilisha maana; eleza maana ya maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine;
Je, Mawazo yaliyotolewa kutoka lugha moja kwenda hadi nyingine; maelezo kutoka lugha
moja hadi nyingine), ukalimani/ufasiri: eleleza maana ya maneno kutoka lugha moja
hadi nyingine, fafanua, uhariri: tengeneza maandishi kwa kuyasahihisha, kuyarekebisha
na kuyapanga kwa ajili ya kuchapa katika gazeti au kitabu, tengeneza. Tahariri, maelezo,
maoni au fikira zinazotolewa na mhariri juu ya jambo fulani katika gazeti, jarida
au kitabu.