2012-11-17 10:03:26

Hazina ya uzee!


Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita hivi karibuni katika nyumba ya Wazee wanaotunzwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ni kati ya matukio ya furaha kwa kundi kubwa la watu linalotambua kwamba, maneno na matendo ya Baba Mtakatifu ni ujumbe tosha kabisa si tu kwa ajili ya kundi dogo la wazee lililobahatika kukutana na kuzungumza naye, bali ni kwa Jamii nzima.

Baba Mtakatifu wakati anawatembelea wazee wenzake aliwakumbusha kwamba, hata Yeye ni mzee anayetambua fika kero, matatizo na ukomo wa maisha ya uzee. Tofauti kabiza na mtangulizi wake, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili aliyezeeka, akateseka kutokana na ugonjwa uliomsababishia wakati mwingine, kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Lakini wazee hao katika umri wao, waendelee kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na wajitahidi kushirikishana mang'amuzi utajiri na hekima ya maisha, kama kitabu ambacho kiko wazi kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya ili waweze kupata dira na mwongozo wa maisha.

Ni maneno ya Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican katika tahariri yake, anayeangalia uzee katika jicho la matumaini kwa kusema kwamba, wazee hawana sababu ya kujitaabisha kujaza utupu wa maisha ya uzee kwa kuwa na mambo mengi ya kutenda, bali watumie busara ya moyo kubainisha mambo msingi na yale ya kawaida; mambo yanayodumu na yale ya mpito! Haya ni mambo yakufanyia haraka hasa ikiwa kama mtu anakabiliwa na ugonjwa na simanzi za maisha ya uzee. Hiki ni kipindi muafaka cha kutafuta ukweli, kwa kumtegemea Aliye juu.

Kipindi cha kuongojea kinaweza kujazwa na maisha ya sala kwa mapana zaidi. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika wazee kusali kwa ajili ya kuombea: maskini, amani pamoja na kusitisha kinzani na migogoro ya kivita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia; anawataka kusali kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni sala yenye nguvu, kwani mzee anayeamini ana matumaini kwamba, yuko karibu na Kristo pamoja na watakatifu wake ambao anawafahamu zaidi, kiasi kwamba, kipindi hiki cha mpito kinakuwa wazi zaidi.

Padre Federico Lombardi anahitimisha tahariri yake kwa kusema kwamba, Jamii inahitaji wazee, kwani inatambua kwamba, wao ni hazina ya utajiri mkubwa; changamoto ya kuendelea kuwahudumia kwa upendo, ili kwa pamoja wote waweze kusema kama alivyosema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa hakika, inapendeza kuwa mzee!







All the contents on this site are copyrighted ©.