2012-11-16 09:58:28

Mwaka wa Imani: Kitabu cha tafakari, maisha ya kichungaji na sala kutolewa kwa wagonjwa na familia zao


Mkutano wa ishirini na saba wa Afya Kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ni fursa makini inayopania kuwajengea uwezo wafanyakazi katika sekta afya ili waweze kushiriki kikamilifu katika azma ya Uinjilishaji Mpya wakitumia Hospitali, Altare ya Mahangaiko ya binadamu kuwa ni mahali muafaka pa Uinjilishaji katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo; utu na heshima ya mwanadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Mheshimiwa Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema, utekelezaji wa dhamana hii unahitaji kwanza kabisa majiundo ya kitaaluma, kiutu na katika maisha ya kiroho, ndiyo maana Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kunako mwaka 1995 lilichapisha Mwongozo wa Wafanyakazi katika sekta ya afya; ukafuatia Waraka wa Kichungaji kutoka kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, Injili ya Uhai.

Baraza mbali mbali ya Kipapa yamekuwa yakitoa pia miongozo itakayowajengea waamini uwezo wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, daima wakijitahidi kufahamu Kanuni Maadili na Mafundisho ya Kanisa kuhusu medani mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameendelea kukazia umuhimu wa mshikamano unaozingatia kanuni ya auni, katika kugawa raslimali ya dunia kwa ajili ya kuwahudumia maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni changamoto pia kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanatumia fursa hii kwa ajili ya kutangaza, kukuza na kuitolea ushuhuda imani yao kwa njia ya huduma makini kwa wagonjwa, wakijali na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wajibu hata kwa wagonjwa wenyewe kutolea ushuhuda wa imani inayoponya na kuokoa pamoja na kuendelea kushiriki katika mateso ya Kristo yanayokomboa.

Padre Chendi anabainisha kwamba, mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, itakayofanyika hapo tarehe 11 Februari 2013, Mama Kanisa atakapokuwa anafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Maadhimisho hayo kwa Mwaka 2013 yatafanyika nchini Ujerumani, kwa kuongozwa na kauli mbiu inayochotwa kutoka katika sehemu ile ya Injili ya Msamaria mwema "Nenda zako, nwe kafanye vivyo hivyo".

Ni changamoto ya kutenda vyema kwa wagonjwa pamoja na kutenda mema kwa mgonjwa anayeteseka kutokana na maradhi yanayomwandama. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahudumu wa sekta ya afya, limeandaa kitabu cha sala ambacho kimekwisha tafsiriwa katika lugha mbali mbali, ili kuwasaidia wahudumu katika sekta ya afya, wagonjwa pamoja na familia zao, kuadhimisha vyema Mwaka wa Imani. Kitabu hiki kina utajiri mkubwa wa tafakari za kitaalimungu, maisha ya kichungaji na sala.

Ni matumaini ya Baraza hili la Kipapa kwamba, kitabu hiki kitatumia vyema na walengwa, kama njia ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano unaojionesha kwa namna ya pekee katika sala, huduma na ushuhuda wa maisha. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kutangaza Injili ya Matumaini na Upendo kwa wagonjwa na familia zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.