Liturujia ya Neno la Mungu: tafakari ya mambo ya nyakati!
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la
Mungu, tukiwa Dominika ya 33 ya mwaka B wa Kanisa. Masomo yanatualika kutafakari juu
ya siku ya mwisho, siku ya hukumu na hivi mwaliko ni kujiandaa mapema, yaani kukaa
tayari. Tunatafakari kuhusu mambo ya nyakati!
Fundisho la
Bwana lisemalo anayetaka kunifuata ajikane nafsi yake mwenyewe, abebe msalaba wake
anifuate kila siku laweza kutusaidia kuelewa kuwa, wajibu wa kuokoka ni wa kila siku.
Lazima kutimiza mapenzi ya Mungu kila siku ya maisha yetu.
Katika somo la
kwanza tunaambiwa juu ya siku ya mwisho yaani siku ya hukumu, siku ya mavuno, siku
ambayo kila mmoja wetu atapata dhawabu ya kazi yake ya kumtumikia Mungu na kutimiza
mapenzi yake. Nabii Danieli anatangaza hali halisi itakavyokuwa siku ile ya mwisho,
yaani kutakuwa na taabu ambayo haijawahi kupata kuonekana lakini kwa wale wote ambao
majina yao yatakuwa kwenye kitabu cha mbinguni basi hawa watapata matunda mema ya
jasho la kazi yao hapa duniani.
Kinyume na hapo ni mateso kwa wale waliojibidiisha
katika kuliishi giza la mwovu na ndiyo kukosa uzima wa milele! Mambo haya yanatisha
lakini basi yanapoletwa kwetu yanatupa tumaini kuwa jasho letu tunalolitoa kwa ajili
ya mapendo hapa duniani litapata matunda hapo baadaye. Ndugu zangu tukumbuke katika
kuishi Imani yetu kuna mateso na madhulumu mbalimbali na hivi yatupasa kuyavumilia
kwa ajili ya uzima wa milele.
Katika Somo la pili tunaendelea kusikia juu ya
Kuhani Mkuu Yesu Kristo aliye mkono wa kuume wa Mungu mbinguni. Yuko huko akingojea
hata wapinzani wake wawekwe chini ya miguu yake. Harudii tena sadaka yake maana mara
moja yatosha kwa ondoleo la dhambi.
Kazi yetu ndugu yangu mpendwa ni kushiriki
ukuhani wa Agano Jipya kwa upendo na unyenyekevu, yaani Misa Takatifu kilicho kile
cha hazina zote takatifu yapaswa kuadhimishwa kwa uchaji na nguvu. Tunapaswa kusikiliza
mafundisho yake kwa njia ya Neno lake na kujenga tabia ya makusudi katika mambo ya
ibada takatifu kwa sifa na utukufu wake.
Mpendwa msikilizaji, Mwinjili Marko
katika sura yake ya 13 anakazia ujumbe uleule wa Nabii Danieli, anatangaza hali itakavyokuwa
nyakati za mwisho. Kutakuwa na giza, nyota za mbinguni kuanguka na mambo kama hayo.
Haya yote ni viashilio tu na hivi siku wala saa hatujui! Kumbe katika hali kama hiyo
mwaliko ni kujitayarisha mapema katika maisha ya kila siku kwa kushiriki hazina zote
za kiroho kadiri Mama Kanisa anavyoziratibisha daima.
Tulilo nalo kwa hakika
ni kwamba Mwana wa Adamu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na kwamba kuna siku ya
mwisho ni hakika, ila ni lini Baba wa Mbinguni pekee ajua jambo hilo! Pamoja na hilo
pia tuna uhakika kwamba waliotenda vema, yaani walioshiriki mateso na msalaba wa Kristu
watafutwa machozi yao kwa kitambaa cha mwanga mtakatifu toka mbinguni.
Mpendwa
unayenisikiliza, yafaa pia kuwa makini, wakati Injili inaandikwa Marko anaadress matatizo
yaliyokuwepo wakati huo na anayalinganisha na mwisho wa dunia, kumbe umakini katika
maisha ya tafsiri ya Neno la Mungu ni muhimu, maana kuna watu wamejiimarisha katika
kutumia maneno haya kutishia watu kwamba mwisho wa dunia uko tayari!
Tafadhali
ajuaye siku na saa ni Mungu peke yake! Kwamba, matatizo yanayozungumzwa katika injili
yako hivi leo katikati yetu si kigezo cha kuweka Neno la Mungu katika mlengo huo wa
vitisho! Neno la Mungu ni kwa ajili ya kutupatia faraja tunapoendelea kukabiliana
na msalaba wa Bwana katika safari ya kwenda mbinguni. Ninakutakia heri na neema za
Kristo mfufuka siku zote za maisha yako tunaelekea kumaliza mwaka B wa Kanisa.