2012-11-15 08:21:16

Mchakato wa Utamadunisho ndani ya Kanisa na vikwazo vyake


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Mheshimiwa Padre Nikodemo Mayala, katika mfululizo wa makala juu ya mchakato wa Utamadunisho Barani Afrika, ambalo kwa hakika ni changamoto endelevu, leo anazungumzia kwa kina na mapana harakati za Utamadunisho katika historia ya Kanisa, vikwazo na changamoto zake. RealAudioMP3

Mahusiano kati ya Injili na Tamaduni. Katika harakati hizi tuzame katika mahusiano ya Injili na tamaduni za watu. Tutazingatia kwa mahususi nyumbani Afrika. Injili ni ithibati hakika ya utamadunisho. Kristo kufanyika mtu alijitamadunisha, aliishi na watu, akafanana nao katika kila kitu isipokuwa dhambi. Alikuja ili amfanye mtu Mungu na Mungu mtu.

Alirejesha sura na mfano wa Mungu- Upendo. Utamadunisho huu wa upendo kamili umetaka turejee tena katika asili yetu ya utakatifu. Hivi, tunahitaji harakati ya kuupokea, kuzingatia na kufanyia kazi. Kristo kwa kufanyika mtu anatupa changamoto za mabadiliko, wongofu, jitihada za kutamaduni na Mungu. Hivi utamaduni wa kweli ni udhihiriko wa upendo wa Mungu kati ya waja.

Injili ya Bwana Yesu imeelezwa na kuwasilishwa katika historia kwa njia ya tamaduni mbalimbali. Simulizi la awali tunakutana na ndugu zetu wayahudi, wayunani, warumi, wazungu. Katika vipindi tofauti utamadunisho ulibainisha fikira mbalimbali na miundo anuwai, wengine walidhani ni civilization-ustaarabu.

Kila aliyekutana na utamaduni mwingine alimwita mwenzie mshenzi, mnyama, mjinga na mpumbavu. Dawa ni kumlevya ugeni, yaani kumgenisha atengane na binadamu wenzake kwa kujenga tabaka, mabwanyenye, vikaragosi na kudharau nyumbani anamozaliwa. Itakumbukwa kuwa wakati fulani ilileta mtafuruku katika Kanisa la awali ikiwalazimu wakutane Yerusalemu.

Ajenda kuu ikiwa watu wawe Wayahudi kwanza kabla ya kuwa Wakristo au wanaweza kuwa Wakristo bila kuwa Wayahudi! Tohara au Kristo?(Mdo.13-15) Kiburi dhambi ya hulka ya mtu ilitawala harakati za utamadunisho wa kimungu na kibinadamu ikazama katika harakati za kinyama na kinyaa.

Unyanyapaa ilikuwa sera bayana. Karipio la Paulo dhidi ya Petro ni mfano uliyo hai: “Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Wayahudi”(Gal.2:14). Aidha, Petro anakiri kuonywa na Mungu: “Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi”(Mdo.10:28). Hivi baadhi walionekana washenzi, wachafu, wasio na utamaduni. Mja na majigambo akaukoloni utamaduni Mungu na kumtweza binadamu mwenzie.

Hatari hii ya kubeza au kutweza tamaduni za watu - tunaweza kufananisha tukio hili na injili kadiri ya Luka sura ya 18:9-14, ndugu zetu wawili wanakwenda madhabahuni mwingine anajidai na kuhesabu kiasi alivyo mwema akimtweza mwingine. Akasahau kuwa daima nyani haoni kundule. Wa pili akaomba radhi na kutambua kuwa yeye ni mtu, si Mungu. Hulka ya uumbaji kwa sura na mfano wa Mungu, wajibu wa kutawala, kutiisha, usawa mbele ya Mungu ni mvuto na mwaliko kwetu kutamadunisha. Kwamba Mungu anajifunua na kudhihirika kati ya watu kadiri ya uelewa wao.

Katika kutamadunisha tendo la Kristo linaloainishwa katika waraka wa mtume Paulo kwa wafilipi 2,6-11. Ni mwaliko na kukumbushwa wajibu wa kutong’ang’ania tamaduni zetu ili kufanikisha uinjilishaji wa kweli wenye msingi katika Imani. Na si kuweka viraka katika Injili.

Ila upenyevu wa Injili katika maisha ya watu. Ndiyo kusema, Injili si kiraka kipya juu ya vazi kukuu, Injili si kiraka chakavu juu ya vazi jipya, Injili ni vazi jipya linalovika tamaduni na watu wote. Kuvaa vazi hili jipya yataka moyo. Kwanza ni changamoto kufasiri, kutafsiri na kuhariri tamaduni zetu, ni kioo cha tamaduni zetu, ni mundu wa kuchenga vitamaduni vyetu, kuchenga vitamaduni hivi ili vipate ladha na manukato mazuri ya Injili.

Daima uzingatiwe wosia wa Kristo : “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza”. Tena, tamaduni zote haziwezi, zinahitaji utimilifu, na utimilifu wake ni Injili, ni Kristo. Ni hakika basi kwamba utamaduni bila Kristo unatindikiwa, utamaduni bila Mungu unachechemea. “wenye afya hawahitaji tabibu bali walio hawawezi” (Mat.9:12). Tamaduni zahitaji tabibu.

Akiingia katika utamaduni wa kiyahudi, Bwana Mkubwa hakuridhika. Mengi yalimwudhi na kutaka mapinduzi na utakaso wa utamaduni haraka iwezekanavyo. Utamaduni huo ulitawaliwa na unyanyaso. Tabaka zilikuwa tabia na haiba yake. Ubaguzi uligawa jumuiya, ndugu walitengana, mkoma, kilema, kiwete kwao hapakuwa kwao alitengwa, kuchangamana na nduguze mwiko. Unyanyapaa huu ulimwudhi Mwenyezi. Ulitia kinyaa ulinuka na kuchafua mazingira. Mungu arejesha upendo. Kristo hakuridhika, akadhamiria ukombozi. “Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake, bali ikifa hutoa mazao mengi”(Yoh.12:24).

Utamaduni una mapungufu. Hakuna utamaduni tuushuhudiwao usiotindikiwa. Una mema, vema, una mabaya, ni mabaya, lazima tuyaondoe. Utamaduni lazima tuuchenge, ndiyo kusema, Utakaso wa tamaduni ni faradhi si hiari. Vile ilivyo suna kwa ugonjwa na faradhi kwa kifo, hali kadhalika, faradhi ya utakaso katika tamaduni zetu. Mwenye kuiona nafsi jamani ataipoteza, mwenye kuipoteza ndugu, hakika ataiona (rej.Mat.10:39).

Utamaduni ni jambo la kihistoria, linaanza, linakuwa kila leo. Hivi daima utatawaliwa na uwezo wa ubongo na wakati. Leo hii tumo katika utandawazi, mwingiliano wa mataifa yote, uhamaji wa watu, mawasiliano, nk. Kila wakati wahitaji maarifa mapya na misingi safi ya maadili.

Uyahudini Mungu alijifunua kwa namna ya pekee katika historia. Lakini uyahudi ule ulitofautiana na uyahudi. Ufunuo haukuwa uyahudi lakini ulimfikia Myahudi kiyahudi. Maandiko yakaenea kwa kiyahudi, mtazamo, fikira, mwono na ukamilifu wote wa kiyahudi. Wayahudi wahamaji na Wayunani wakahitaji ufunuo huo, nao ukawasilishwa katika mtazamo huo uhamishoni. Myahudi –Myunani akafasiri ufunuo kiyahudi – kiyunani. Myunani akafasiri kadiri ya falsafa yake ya maisha na maarifa.

Fikira na mtazamo wao ulibainisha ufunuo huo katika uelewa wao. Hatimaye utawala wa kirumi ukakutana na ufunuo. Nao ukafasiri kuwa ni lazima ya watu wote kuufahamu. Ikapoteza mweneo na mwasilisho wa wongofu likawa jambo la kisiasa na fasheni. Watu wakakristishwa kwa amri, kwa upanga. Uhuru katika Kristo ukafa. Wakarudi utumwani. Injili ikawa sababu ya utumwa, ladha ya ukombozi ikafishwa, kama kuzima mshumaa. Lakini haikuwezekana milele.

Watu wakatawanyika na kugawanyika. Marufuku ya kutafakari Neno ikabeza wongofu wa kweli. Watu wakawa kama vipere ama bendera. Njaa na kiu hii ikazaa utitiri wa vi dini na rundo la madhehebu. Sasa kumekucha, tongotongo zinatoka.








All the contents on this site are copyrighted ©.