2012-11-15 14:14:04

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaodai wongofu wa ndani na ushuhuda amini miongoni mwa Wafuasi wa Kristo


Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anaendelea kukazia umuhimu wa majadiliano ya kiekumene kama mtindo wa Uinjilishaji mpya. Huu ndio mwendelezo ulioneshwa kwa namna ya pekee na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji mpya iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican. Ndiyo mada ambayo pia imeongoza mkutano wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji umoja wa Wakristo, uliohitimishwa kwa kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita mjini Vatican, siku ya Alhamisi, tarehe 15 Novemba, 2012.

Mwaka wa Imani unakwenda sanjari na kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ambamo Mababa wa Mtaguso walikazia kwa namna ya pekee, dhamana ya Uinjilishaji sanjari na jitihada za kujenga umoja miongoni mwa Wakristo, ili wote wawe wamoja kadiri ya utashi wa Kristo, kwani utengano ni kashfa kubwa kwa Wakristo duniani na una athari kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji.

Wakristo hawana budi kuongeza juhudi za kujipatanisha kama alivyotaka Kristo mwenyewe katika ile sala ya kikuhani, ambayo anakazia umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wake, ili dunia iweze kuamini kwamba, ametumwa na Baba yake wa mbinguni. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Uinjilishaji na ushuhuda unaofumbatwa katika Umoja wa Wakristo.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati alipokutana na wajumbe wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo, anayeendelea kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo, kama kielelezo makini cha kutangaza Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Watu wana kiu ya maisha ya kiroho, wanakabiliana na umaskini wa kiroho, kiasi kwamba, wanashindwa kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Hii ni changamoto kwa wakristo wote kuzima kiu hii ya maisha ya kiroho, kwa kuonesha njia inayojikita katika ushuhuda wa imani kwa Mungu aliye hai; anayefahamu na kupenda, ambaye yuko karibu na waja wake; Mungu anayesubiri kwa uvumilivu mkubwa jibu la upendo kutoka kwa mwanadamu katika hija ya maisha yake ya kila siku. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu kwa Wakristo wote kuchangamkia utangazaji wa Injili ya Kristo kwa watu wa ulimwengu mamboleo.

Ni ushuhuda unaomwonesha Mungu ambaye amejifanya jirani kwa binadamu kwa njia ya Yesu Kristo, dhamana ya kuchuchumilia umoja na mshikamano miongoni mwa wafuasi wa Kristo, wanaotambua kwamba, wanaunganishwa pamoja kwa njia ya Imani kwa Mungu, Baba na Muumba, aliyejifunua kwa njia ya Yesu Kristo, akawakirimia waja wake Roho Mtakatifu anayetakatifuza na kujenga. Hii ndiyo imani ya Ubatizo ambayo waamini wameipokea katika matumaini na mapendo, wanayoweza kuiungama kwa pamoja.

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kitaalimungu, dhamana ambayo Kanisa Katoliki linaipatia kipaumbele cha pekee, ingawa bado kuna njia ndefu ili kuweza kufikia umoja kamili. Hija ya majadiliano iwawezeshe waamini kushirikishana utajiri na mang'amuzi ya maisha ya kiroho na kweli za kitaalimungu, ili kuhamasisha ushuhuda wa imani.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, wakristo wanapaswa kujitoa kimaso maso katika kudumisha umoja miongoni mwao, lakini watambue kwamba, hizi si juhudi zao binafsi, bali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inaweza kupatikana kwa njia ya Yesu mwenyewe kwani Kanisa ni lake. Kumbe, Uinjilishaji mpya ni mwaliko wa kutembea pamoja kwa kurekebisha kasoro na misigano ili umoja wa kweli uweze kuonekana.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwamba, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, utasaidia pia kukuza na kukoleza majadiliano ya kiekumene, umoja na imani kama njia ya ushuhuda amini kwa wale wasiomwamini Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu au wale ambao wamemezwa zaidi na malimwengu licha ya kubahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa maishani mwao. Majadiliano ya kiekumene kwanza kabisa ni kutambua kazi ya Mungu, kwa uvumilivu na unyenyekevu wa hali ya juu kwa kupania kutekeleza mapenzi ya Mungu.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaodai wongofu wa ndani na utashi wa kumfuasa Kristo pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.