Changamoto zinazojitokeza katika kuendesha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu Barani
Afrika
Monsinyo Pius Rutechura Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki
na Kati, CUEA, katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha changamoto kadhaa wanazokabiliana
nazo katika harakati za kuendesha taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki
Afrika Mashariki, lakini kwa namna ya pekee, CUEA.
Anasema, wanapaswa
kuwa macho na makini katika kuandaa na kuendesha programu za masomo zinazokidhi mahitaji
ya elimu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; programu
ambazo zinapania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kutokana na myumbo
wa uchumi kimataifa, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu havina budi kuhakikisha
kwamba, vinatafuta vyanzo mbali mbali vya fedha nje ya karo inayotolewa na wanafunzi,
ili kuweza kufanya maboresho zaidi katika mfumo wa elimu inayotolewa vyuoni hapo.
Juhudi hizi ni sehemu ya mchakato wa kutaka kujitegemea kwa kiasi kikubwa.
Katika
ulimwengu mamboleo, hatoshi kuwa na cheti, bali Jamii inaangalia zaidi ubora na viwango
vya elimu inayotolewa chuoni hapo, ili kukabiliana na ushindani unaojitokeza katika
taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia. Ubora lazima ukidhi
viwango vya kitaifa na kimataifa sanjari na kujenga ushirikiano wa dhati na vyuo vingine.
Monsinyo
Rutechura anasema kwamba, kuna haja ya kubadilisha mtindo wa uongozi kwa kujikita
zaidi katika ushirikiano na umoja; utunzaji bora wa kumbu kumbu pamoja na viongozi
wenyewe kujiamini kwamba, wanaweza kutekeleza dhamana waliyokabidhiwa na Kanisa pamoja
na Jamii katika ujumla wake. Yote haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ili
kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuka siku hadi siku katika
sekta ya elimu ya juu.