2012-11-14 08:20:04

Wainjilishaji, jiinjilisheni kwanza, ili muweze kuwainjilisha wengine kwa umakini mkubwa zaidi!


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, yawe ni fursa muhimu sana kwa waamini, lakini zaidi kwa viongozi wa Kanisa kuweza kuikimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili Sakramenti hii iweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha kwa viongozi wenyewe na wale ambao Mama Kanisa amewapatia dhamana ya kuwaongoza. Lengo kuu ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Sakramenti za Kanisa.

Ni maneno ya Kardinali Timothy Dolan, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, alipokuwa anafungua mkutano wa Maaskofu mapema juma hili. Maaskofu wanatambua taabu na mahangaiko ya watu wao yaliyojitokeza hivi karibuni kutokana na tufani, changamoto za Uinjilishaji Mpya kama zilivyobainishwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya, Fursa mbali mbali za kukuza, kuimarisha na kutolea ushuhuda imani pamoja na umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni.

Kanisa linakabiliana na changamoto pevu ya kuendelea kusimama kidete kwa kupaaza sauti yao ya kinabii, katika kulinda na kutetea Injili ya Uhai, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, utu na heshima ya mwanadamu, bila kuwasahau wale ambao bado wanaogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na njaa. Bado kuna kundi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaopaswa kulindwa na kutetewa haki zao msingi na kwamba, Kanisa lina wajibu wa kusikiliza kilio cha watu wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia sanjari na kuimarisha uhuru wa binadamu.

Kardinali Dolan anawakumbusha Maaskofu kwamba, wao kama viongozi wa Kanisa, wanapaswa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo, wakitambua kwamba, kwao Yesu ni: Mwana wa Mungu, Mkombozi wa dunia, rafiki na mwenza katika hija ya maisha, kwani alikwisha kusema kwamba, Yeye ni njia, ukweli na uzima, mwaliko kwa wafuasi wake kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na mengine watapewa kwa ziada.

Yesu anapaswa kuwa ni kiongozi wao katika mchakato wa majadiliano ya: kitamaduni, kidini na kiekumene, daima wakijitahidi kutubu na kuongoka, kama changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya, kwani Uinjilishaji mpya unawachangamotisha kujiinjilisha kabla ya kuwainjilisha wengine, ili kweli Injili ya Kristo iweze kupata nafasi katika maisha ya watu wa ulimwengu mamboleo.

Mihimili ya Uinjilishaji haitaweza kuvuna matunda mengi anakumbusha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ikiwa kama wao wenyewe hawatachukua hatua madhubuti za Kujiinjilisha kwanza. Maaskofu katika maisha na utume wao, lazima wachuchumilie toba na wongofu wa ndani, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vinavyohamasisha upya wa maisha yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo. Ili changamoto hii iweze kufanikiwa, kuna haja ya kufufua na kuimarisha moyo na ari ya kutaka kupokea Sakramenti ya Upatanisho mara kwa mara.

Kardinali Dolan anasema, kwa hakika Sakramenti ya Upatanisho ni kwa ajili ya wainjilishaji, ili waweze kujiinjilisha na hatimaye, kuwainjilisha wengine, ili waweze kukutana na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, anayewaonjesha huruma na upendo wake; Yesu anayewaalika kutubu na kuongoka, ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili.

Sakramenti ya Upatanisho ni changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wajitahidi kuipatia kipaumbele cha pekee, kwa kutambua umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa hakika Sakramenti ya Upatanisho ni Sakramenti ya Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.