2012-11-14 08:40:25

Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika kukutana kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2012, Kusini mwa Italia


Kwa mara ya kwanza Baraza la Maaskofu Kanda ya Afrika ya Kaskazini, litakuwa na mkutano wake wa kawaida Jimboni Mazara del Vallo, Kusini mwa Italia, kwa mwaliko wa Askofu Domenico Mogavero, kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Novemba 2012.

Askofu Mogavero mara mbili, ameshiriki katika mkutano wa Baraza la Maaskofu Kanda ya Afrika Kaskazini kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu wanaotoka Afrika ya Kaskazini Jimboni mwake, wengi wao wakiwa ni waamini wa dini ya Kiislam. Maaskofu wataanza mkutano wao kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani, itakayofanyika Jumapili tarehe 18 Novemba 2012. Lengo la mkutano huo Jimboni hapo ni kuweza kubadilisha ujuzi, uzoefu na mag'amuzi ya shughuli za kichungaji.

Kwa upande wake Askofu mkuu Vincent Landel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kanda ya Afrika ya Kaskazini, anasema, wanekubali mwaliko kutoka kwa Askofu Dominico Mogavero kwa kutambua kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wanaotoka Libya, Tunisia na nchi kadhaa za Afrika ya Kaskazini ambao wamekimbilia Kusini mwa Italia kwa ajili ya usalama wa maisha yao. Kusini mwa Italia limekuwa ni eneo kwa ajili ya wakimbizi wengi kutoka Afrika Kaskazini.

Mkutano huu unafanyika nchini Italia, wakati ambapo wanasiasa wengi kutoka Ulaya wanaendeleza sera za ubaguzi na kandamizi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, uwepo wa Maaskofu Katoliki Kanda ya Afrika Kaskazini ni alama na kielelezo cha kuthamini na kujali mahangaiko yao, wanataka kushirikisha ujuzi, mang'amuzi pamoja na matarajio yao kwa wahamiaji na wageni kutoka Afrika ya Kaskazini.

Katika mkutano wao, Maaskofu hao kwa pamoja wataangalia pia changamoto za Uinjilishaji Mpya Kaskazini mwa Afrika, dhamana inayotekelezwa kwa njia ya majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam.

Askofu Domenico Mogavero, mwenyeji wa mkutano wa Maaskofu Katoliki Kanda ya Afrika ya Kaskazini anabainisha kwamba, lengo lake ni kutaka kujenga umoja na mshikamano katika shughuli za kichungaji, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kupata huduma muhimu katika maisha yao; kwa kuimarisha mwingiliano wa tamaduni za watu wanaoishi katika Ukanda wa Bahari ya Mediterranea, katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.