Lengo la Uinjilishaji Mpya katika Ulimwengu mamboleo
Mpendwa msiklizaji wa Radio Vatican, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu kabisa katika
mfululizo wa vipindi vyetu vya uinjilishaji wa kina ambapo tunaendelea kuiangalia
kwa pamoja Mwongozo wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa
hivi karibuni. Juma hili tupige hatua mbele kidogo kuangalia juu ya kukutana na kuungana
na Kristo ambalo ndilo lengo msingi la uinjilishaji.
Baba Mtakatifu
Benedikto XVI anakumbusha kwa mara nyingine tena juu ya utume msingi wa Kanisa lilipokea
toka kwa Kristu mwenyewe yaani kuhubiri injili kwa mataifa yote na kuwafanya wote
kuwa wanafunzi wa Yesu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI analikumbusha Kanisa kuwa Utume
lililokabidhiwa na Yesu mwenyewe kimsingi ni utume unaolidai na kulituma Kanisa kuihubiri
na kuifundisha Injili kama Yesu mwenyewe alivyoihubiri akingali katika ulimwengu huu.
Tena analifananisha Kanisa na Mtume Paulo ambaye alisema wazi kuwa yeye ni
Mtume aliyewekwa wakfu na Yesu Mwenyewe kwa ajili ya kutangaza ujumbe wa Kristo. Hivyo
anamalizia Baba Mtakatifu kuwa kazi ya Kanisa si kufundisha Biblia au vifungu vyake
bali kuutangaza ujumbe wa Kristo katika namna kwamba watu wa Mungu waweze kuuishi
ujumbe huo.
Injili, Baba Mtakatifu Benedikto XVI anafafanua kuwa ni Kristu
mwenyewe anayeongea na watu wake ndani ya Kanisa. Kumbe Kanisa lina utume wa kumtangaza
Kristu anayejidhirisha siku hadi siku katika neno lake daima akiwaonesha watu wake
njia sahihi ya kuenenda, akiwaokoa kwa lile tumaini analolitoa katika neno lake juu
ya ufalme wa Mungu na kuwapatia uzima wa milele pale watu wake watakapomsikia na kumwendea
yeye.
Kwa msaada na maongozi ya Roho Mtakatifu wampokeaye wale wanaomsikia
Kristu na kumwamini wanapata uzima na kuokoka na yule mwovu na kuwa mashahidi wa Kristu
kwa wengine.
Kuhubiri Injili kumbe ni kujenga mazingira, mahali na mwanga kwa
wanafamilia ya Mungu kumjua Kristu, kumpokea katika maisha yao kama Bwana na Mwokozi
wao, kumpenda na kumtumikia yeye siku zote. Kwa maneno mengine ni kujenga mazingira
mazuri ya watu wa Mungu kukutana uso kwa uso na Yesu katika neno lake na sakramenti
zake na kuungana naye kabisa katika Imani. Waamini kwa uinjilishaji mpya wanapaswa
kuwezeshwa kukutana na Yesu katika neno lake na kuungana naye katika Ekaristi Takatifu.
Makutano
haya baina ya muumini na Yesu mwenyewe ni nafasi pekee ambapo waumini wanapata kwa
nguvu ya Roho Mtakatifu kuonja muungano wa Yesu na Mungu Baba. Yesu anamdhihirisha
Baba kwa viumbe wake na tena anawaleta wafuasi wake kwa Baba. Katika mapana yake Uinjilishaji
mpya ni ujenzi wa mazingira kwa utangazi wa imani ambayo si inafikiriwa tu bali waamini
wanaishuhudia kwa maisha yao ya kila siku, wanaiadhimisha katika ibada, wanaisali
na kuuiishi katika mazingira halisi ya ulimwengu huu wa leo.
Baba Mtakatifu
Benedikto XVI anakazia na kulitaka Kanisa kujifunga kibwebwe katika suala zima la
uinjilishaji mpya na hivyo anawataka Maaskofu katika Sinodi kujipanga vizuri kwa zoezi
hili. Anasema kutanga imani ni jambo kubwa linaloleteza wajibu mkubwa kwa upande wa
watangazaji wa imani. Kanisa halina budi kuwa mfano wa maisha ya imani, maisha ya
ushuhuda wa ujumbe wa Kristo.
Baba Mtakatifu anasema sio rahisi kutangaza
imani kwa wengine wakati mtangazaji mwenyewe haamini na haishi kulingana na imani
anayoitangaza. Hivyo changamoto kwa Kanisa kujizatiti kiimani na kimapendo yaani kumvaa
Kristu mwenyewe ili likisimama na kupunga bendera ya Kristu basi lionekane kweli mpiga
debe wa Kristo.
Anaendelea kubainisha kuwa utume huu wa kutangaza imani ueleweke
vizuri miongoni mwa wanakanisa hivi kwamba kila mbatizwa ahusike moja moja katika
uinjilishaji mpya. Maana yake hizi si zama za kusimama mimbarini bali kumtangaza Kristo
kwa maisha ya ushuhuda: kwa matendo yetu ya imani na upendo tumdhihirishe Kristo kwa
mataifa yote.
Kanisa linaalikwa kupitia waumini wake kuushuhudia upendo upeo
wa Kristo usio na mipaka kwa mataifa. Kile alichofanya Yesu mwenyewe ndicho wanakanisa
wanapaswa kukiendeleza katika ulimwengu wa leo; kufukuza pepo wachafu, kuponya magonjwa
na kuwajali wahitaji wa kila hali.
Mpendwa msikilizaji hadi hapa tumefika mwisho
wa kipindi chetu kwa siku ya leo. Nakutakia kila Baraka na kheri kutoka kwa Mungu
Baba, nikikuaga kutoka studio za Radio Vatican ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako
Padre George wa Bodyo.