2012-11-14 08:57:42

Kipimo mama katika mchakato mzima wa utamadunisho ni: Kristo, utu, heshima na haki msingi za binadamu


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Mheshimiwa Padre Nikodemo Mayala katika makala juu ya Utamadunisho, sehemu ya kwanza amegusia baadhi ya mambo yanayounda dhana ya utamaduni na changamoto zake kwa ajili ya kukoleza mchakato wa utamadunisho, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee, na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Afrika. RealAudioMP3

Kimsingi hii inapaswa kuwa ni changamoto endelevu. Ili kuweza kujikita katika mchakato huu, leo Padre Mayala anaendelea kuchambua mambo kadhaa kama ifuatavyo:

Sheria, Taratibu na Mwongozo wa maisha ya kila leo. Namna ya kutenda, kuhusiana na kanuni anuwai zinazojenga na kuinda kila leo. Ni mpango utumikayo kufanya jambo fulani. Mwinjili Matayo anabainisha kuwa mambo makuu ya sheria ni adili, na rehema na imani (Mat.23:23). Utamadunisho walenga kuyazingatia mambo makuu ya sheria. Mambo ambayo yanajenga utawala wa Mungu, yanatimiza kazi ya ukombozi wa Mwanadamu na kutakatifuza malimwengu.

Kisasili/visasili, yaani hadithi inayoeleza/zinazoeleza asili ya watu, matukio, nk. Kwa hulka yake visasili vimebuniwa, ni kazi ya ubunifu kueleza asili ya watu, jambo au kitu – mathalani, kuhusu mahuluku, dhambi ilivyoingia ulimwenguni, nk. Ni hadithi zinaleta ukweli fulani katika asili na maisha.

Kipimo mama ni Kristo.

Kazi ya utamaduni. Kuarifu, kupasha habari, kujulisha. Utamaduni wafasiri na kutafsiri mfumo na kanuni za utakatifu na maisha ya watu. Utamaduni huwasilisha ujuzi, utambulisho wa watu. Kwa utambulisho namaanisha ithibati tambulishi na tenganishi. Yaani, ndiyo na hapana. Mimi ni mwafrika, mimi si mzungu, mimi si mwasia, mimi si mwamerika, mimi si mwaustralia. Hii ndiyo kusema, utamaduni ni tambulishi na tenganishi.

Safari ya utamadunisho ni jadi asilia ya binadamu. Mahuluku yanathibitisha ukweli huu kuwa mtu, mazingira na juhudi ni za lazima ili kuishi kwa wakati. Jana si leo, leo si kesho. Wala leo si jana na kesho si leo. Ingawa kesho lazima iitambuwe jana, na kesho lazima iikiri leo.

Ndiyo kusema, katika harakati za utamadunisho tunatambua wakati na changamoto ya mapishi au historia katika kutuunda. Maana wahenga wanatukumbusha kuwa “asiyeijua historia yake anabaki mtoto”. Utamaduni ni mhunzi wetu tunaelea kwa sababu tuliundwa na tunaundwa. Yakini ni vema kuikiri jana iliyotuunda na leo inapotuunda na kuboresha hali yetu, tupate kujenga utawala wa Mungu. Utamaduni wawatambulisha watu. Utamadunisho ni jawabu sahihi kuwatambulisha watu wa leo. Watu hujulikana kwa tamaduni zao.

Mathalani, ukarimu ni jadi ya Afrika, mgeni ni baraka; wageni hupokelewa bila kubaguliwa, hata wakijibagua hawafukuzwi, ardhi watapata, kazi watapata, heshima watapata, utu wao utathaminiwa, daima wataitwa kwa majina yao: mzungu ataitwa mzungu, si mdori, mwingireza ataitwa mwingireza, muitaliano ataitwa mwitaliano, mjerumani ataitwa mjerumani. Atatambuliwa kwa heshima na tamaduni za taifa lake. Habezwi, hatwezwi, anaheshimiwa. Na mnyamahanga ataitwa kwa jina si kwa kundi.

Familia ni tunu dhahabu. Familia ikikosa mtoto ndoa iko hatarini. Watoto hawanyongwi tumboni, wala hawachaguliwi tumboni. Jambo la msingi ni mtoto. Kwamba familia ile ina mtoto. Familia ile ina malezi safi. Utamaduni mfu wa sasa: vitanzi, dawa vizuia mimba, sindano depo provera, uhuru huria. Hii si familia ya kiafrika. Familia ya kiafrika inazingatia: baraka ya watoto, watoto ni baraka, ithibati ya uwepo wa familia.

Malezi: Familia bila malezi si familia ya kiafrika. Msemaji, familia ya kiafrika ina msemaji baba au mama, wengine wanapaswa kusikiliza, kujifunza mila na desturi njema toka kwa wazazi. Utii si jambo la kufikirika, si nadharia ni maisha ya mwafrika. Nidhamu inatunzwa, familia inakuzwa, familia ni pana. Familia ilienzi udugu. Sote ni ndugu. Umimi si asili ya familia ya kiafrika. Familia ya kiafrika ni sisi. Familia yetu, si familia yangu.

Hivi Injili iingie kwenye familia hiyo yenye udugu, yenye kuenzi maisha, yenye nidhamu, utii, utaratibu, usikivu, mwongozo. Mkubwa alitambulika kwa umri, busara, hekima, wajibu, uongozi mzuri, heshima. Kwa jina jingine huyu aliitwa mzee, hata kijana hakunyimwa hadhi ya uzee. Mali haikuwa heshima bila maadili.

Kumbe, maadili mema ndiyo kipimo cha nafasi katika jamii. Leo ni mali, fedha, kisomo, dawa za kulevya, kuavya, kuua watoto wangali tumboni, u changudoa, ufisadi, utalii. Injili ipenye na kuzama katika maadili ya kiafrika. Si maadili ya demokrasia ya kuruhusu mafisadi wa imani, walanguzi wa uchumi, walanguzi wa mapenzi, watapeli wa siasa, vibaraka. Hapendwi mtu, kinapendwa kitu!








All the contents on this site are copyrighted ©.