Vyuo vikuu vya Kikatoliki vinavyojipanga kucharuka katika maboresho ya viwango vya
elimu sehemu mbali mbali za dunia!
Monsinyo Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki
na Kati, CUEA ni kati ya wajumbe kutoka vyuo vikuu vya kikatoliki walioshiriki katika
mkutano wa wakuu wa vyuo hivi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mkutano wa wakuu
wa vyuo vya kikatoliki uliwakutanisha na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki ili kubainisha
mwelekeo wa vyuo vikuu vya kikatoliki katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.
Wamepata
nafasi ya kuweza kufafanua kwa kina na mapana utambulisho wa vyuo vikuu vya kikatoliki,
taswira, malengo na utume wake ndani ya Jamii husika. Wamegusia ubora na viwango vinavyotakiwa,
kwa kuzingatia na kuheshimu: maadili, kanuni, urithi na Mapokeoa ya utamaduni wa utoaji
wa elimu kutoka katika vyuo vya kikatoliki sehemu mbali mbali za dunia.
Imekuwa
ni nafasi ya pekee anasema Monsinyo Rutechura kwa wajumbe kupembua jinsi ambavyo vyuo
hivi vinaendelea kutoa elimu ya juu, usimamizi na maandalizi ya wale wenye dhamana
ya maboresho ya viwango na ubora wa elimu ya juu. Kila Chuo kilipata nafasi ya kuangalia
programu zake, vianzio vya fedha katika jitihada nzima za kutaka kujitegemea, maboresho
katika mfumo wa uongozi, ili uweze kukidhi mahitaji na matarajio ya watu wa Karne
ya ishirini na moja.
Wajumbe kwa pamoja, wamekazia umuhimu wa kudumisha na
kuendeleza mshikamano wa kimataifa ili kusonga mbele katika harakati za kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la ujinga, umaskini na magonjwa.