Utawala bora, misingi ya maadili na utu wema ni dawa mchunguti katika mapambano dhidi
ya rushwa, ufisadi na ubiafsi
Utawala bora na makini unaozingatia na kuheshimu sheria, kanuni na maadili ni muhimu
sana katika mapambano dhidi ya adui ujinga, umaskini na magonjwa. Ni kinga madhubuti
inayowajengea watu moyo wa mshikamano, unaopania kulinda na kudumisha misingi ya haki,
amani, upendo, daima wakijitahidi kutafuta mafao ya wengi na maendeleo endelevu.
Uwajibikaji
katika kutafuta mafao ya wengi ni jambo la msingi sana wakati huu ambapo nchi nyingi
zinaendelea kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Ubinafsi, ukiukwaji
wa maadili, miiko ya uongozi na utawala bora umepelekea kuibuka kwa kinzani na migogoro
ya kisiasa kati ya "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi na wale wanaosema, eti ponda
mali kufa kwaja!". Matokeo yake rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali ya umma vinaendelea
kuwa ni saratani ambayo itachukua muda mrefu kupata tiba yake, ikiwa kama viongozi
hawathubutu kufanya maamuzi machungu kwa kuwawajibisha wale wanaokiuka kanuni, taratibu,
miongozo na maadili ya nchi.
Pengine umefika wakati wa kuwajibisha badala
ya kufumbiana macho kama sera ya kulindana wakati ambapo nchi nyingi zinaendelea kuteteketea
kwa ubinafsi na uchoyo!