Papa atangaza nia binafsi ya kuanzisha Taasisi Mpya ya Lugha ya Kilatini
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa utashi wake mwenyewe, ameanzisha Taasisi
ya Lugha ya Kilatini, kwa kutambua umuhimu wake ndani ya Kanisa Katoliki, tangu wakati
ule wa Pentekoste, waamini wa Kanisa la Mwanzo walipokuwa wanazungumza lugha mbali
mbali, lakini wakaelewana.
Tangu awali, anasema Baba Mtakatifu katika Waraka
unaonesha nia yake ya kuanzisha Taasisi ya Lugha ya Kilatini kwamba, lugha ya Kigiriki
na Kilatini zimekuwa zikitumiwa na Mama Kanisa katika mawasiliano. Baada ya kutoweka
kwa Himaya ya Kirumi, Kanisa Katoliki likaendelea si tu kutumia lugha ya Kilatini,
bali likawa ni msimamizi na mhamasishaji wake mkuu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi
cha kutumika katika taalimungu. liturujia, majiundo na urithishaji wa maarifa.
Hata
leo hii anasema Baba Mtakatifu, Lugha ya Kilatini ina umuhimu wake kwa watu na tamaduni
mbali mbali, kwani ni chemchemi ambayo watu wasomi na wanazuoni wanakwenda kuzima
kiu yao ya ufahamu na bado inaendelea kutumika katika masomo ya Falsafa na Taalimungu
kwa ajili ya Mapadre wa baadaye. Wasomi wengi wanaendelea kukuza ari ya kutaka kujichotea
utajiri wa unaofumbatwa katika lugha ya Kilatini katika masuala ya sayansi na teknolojia.
Huu ndio mwelekeo mpya unaojionesha katika ulimwengu mamboleo kwa kuwahusisha
vijana wengi zaidi kutoka katika tamaduni mbali mbali duniani. Ndiyo maana anasema
Baba Mtakatifu kuna haja ya kuwachangamotisha watu wengi zaidi kupenda kujifunza na
kuifahamu lugha ya Kilatini katika mazingira ya Kanisa na katika tamaduni mbali mbali,
kwa kuwa na mbinu makini za ufundishaji ili kuunganisha nguvu na taasisi nyingine
zinazojikita katika ufundishaji wa lugha ya Kilatini, bila kuwasahau wasomi wanaoitumia
lugha hii.
Lengo ni kuonesha kipaumbele cha pekee katika utajiri unaofumbatwa
kwenye utamaduni wa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anafuata
nyayo za watangulizi wake ili kufanikisha lengo hili, ndiyo maana kwa utashi wake
mwenyewe ameamua kuanzisha Taasisi Mpya ya Lugha ya Kilatini, itakayokuwa chini ya
usimamizi wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Itaongozwa na Rais pamoja na Katibu mkuu
watakaoteuliwa na Baba Mtakatifu mwenyewe pamoja na Baraza la Elimu.