2012-11-13 08:31:53

Mkutano wa 27 wa Afya Kimataifa kufanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 15-17 Novemba 2012


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema kwamba, kuanzia tarehe 15 hadi 17 Novemba 2012 kutafanyika mkutano wa ishirini na saba wa afya kimataifa hapa mjini Vatican, kufuatia maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na changamoto zilizotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya iliyohitimishwa hivi karibuni.

Anasema, Kanisa linatambua na kuthamini utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwaponya watu kutokana na maradhi yanayowasumbua, kama sehemu ya mwendelezo wa kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe. Hii ndiyo changamoto iliyopelekea hata Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kuamua kuanzisha Baraza la Kipapa la huduma kwa wahudumu wa sekta ya afya.

Hili limekuwa ni Jukwa la upendo ambalo limetumiwa na watakatifu na watu wenye mapenzi mema katika mchakato wa kumhudimia mwanadamu: kiroho na kimwili kwa njia ya karama na utume wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa.

Leo hii Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa katika sekta ya afya, kwani linamiliki na kuendesha Hospitali laki moja na ishirini, sehemu mbali mbali za dunia. Ni Kanisa ambalo linajitahidi kutoa huduma makini hata vijijini, kama sehemu ya mtandao wake wa kutangaza Injili ya Upendo, kwa wagonjwa kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kusema kwamba, Kanisa litaendelea kutoa huduma ya upendo kwa binadamu katika mahitaji yake: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anasema kwamba, kutokana na changamoto hii endelevu, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahudumu wa sekta ya afya, litakuwa na mkutano wa afya kimataifa, utakaoongozwa na kuli mbiu "Hospitali kama mahali pa Uinjilishaji: utume wa kibinadamu na kiroho".

Hii ni changamoto endelevu kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto ya kuendeleza mchakato wa kutangaza Imani ya Kikristo, kama walivyosisitizia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba, hali ambayo pia inaibua changamoto na matatizo ya kimaadili na utu wema, wakati mwingine, utu na heshima ya binadamu viko hatarini.

Mama Kanisa anawaalika wahudumu katika sekta ya afya, kumwangalia, kumheshimu na kumhudumia kila mgonjwa kwa heshima na nidhamu ya hali ya juu, wakitambua kwamba, wanaendeleza ile dhamana na utume wa Yesu Kristo, Msamaria mwema anayemganga mwanadamu kwa divai ya upendo na mafuta ya faraja.

Kwa vile Kanisa ni mdau mkubwa katika sekta ya afya, anayo haki kupata ruzuku kutoka Serikalini na Taasisi za Kimataifa, ili liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Jamii kwa kutambua kwamba, ni huduma kwa wote bila ubaguzi na inapania kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si mahali pa biashara.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anasema kwamba, mkutano wa ishirini na saba wa afya kimataifa, utajikita zaidi na zaidi katika masuala ya: kitaalimungu, kiutu na kibinadamu; tema zitakazochambuliwa kwa kina na mapana na wataalam katika sekta ya afya; maisha ya wagonjwa hospitalini. Historia na utume wa Kanisa; Maadili na ubinadamu; tasaufi na huduma ya upendo, ndiyo mwongozo utakaotumiwa na wajumbe wakati wa mkutano huu unaotarajiwa kufungwa rasmi hapo jumamosi tarehe 17 Novemba 2012.

Hospitali kama sehemu ya Uinjilishaji ni mada itakayochambuliwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji Mpya. Utakuwa ni wajibu wa Askofu mkuu Protas Rugambwa, katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuratibu majadiliano kuhusu Hospitali za Kikatoiki katika ulimwengu unaobadilika haraka.

Ni majadiliano yatakayochota hisia, mang'amuzi, ujuzi na uzoefu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa lengo la kutaka kutajirishana kama sehemu ya utoaji wa huduma makini kwa wagonjwa. Bara la Afrika litawakilishwa na Askofu Joachim Muyinga kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa UKIMWI.

Mfuko wa Msamaria Mwema, ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili, kwa kushirikiana na wafadhili mbali mbali utatoa msaada wa vifaa vya Hospitali zilizoko Butembo, Kivu ya Kaskazini, nchini DRC. Baraza la Maaskofu Katoliki litapatiwa pia dawa za kurefusha maisha kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI nchini Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.