2012-11-13 07:51:42

Kanisa Barani Afrika na changamoto za Utamadunisho


“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati na Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Mat.5:17). RealAudioMP3

KANISA NYUMBANI : UTAMADUNISHO NA CHANGAMOTO ZAKE

Utamaduni, ni mila, asili, jadi na desturi za kundi la jamii Fulani. Ni hulka ya maumbile ya watu au jamii husika. Hii yagusa maisha ya kila siku, utaratibu, miongozo, maendeleo, mwono na mtazamo. Hivi utamadunisho ni kumsimika mtu kikamilifu katika yeye anapokutana na kitu kingine au jamii nyingine. Si kumgenisha. Mcheza kwao hutuzwa!

Mambo yanayoeleza utamaduni.
Lugha: mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa fulani au kabila fulani kwa ajili ya kuwasiliana; maneno na matumizi yake; mtindo anaotumia mtu kujieleza.

Msamiati, misemo, methali, vitendawili, nyimbo, ngoma, ishara, ngano, nk. Lugha hutawala namna watu wanavyoufinyanga/wanavyouumba ulimwengu wao (Nadharia tete ya Sapir na Whorf). Katika kutamadunisha twahitaji lugha. Afrika ni lugha ipi itumike? Ya mkoloni au ya mkazi? Kisukuma au kichaga, kihaya au kinyakyusa, kiibo au kiyoruba, kinyankolo au kiluo! Tanzania ni kiswahili.

Kumbe, tutakuwa na mawasiliano katika kiswahili, tafsiri katika kiswahili, fasiri katika kiswahili, utafiti katika kiswahili. Lakini kiswahili kimeundwa na wabantu. Tena tutachungua mila na desturi anuwai za utakatifu na maisha ya wabantu, tutatafiti Biblia kutoka katika lugha za asili (kiaramayo, kiebrania, kiyunani, kisiria) na mapokeo ya Urithi wa kitume na kuchungua na kuhariri msamiati sahihi katika lugha ya wakazi, Kibantu, kwetu kiswahili.

Barani Afrika hadi leo lugha rasmi za mawasiliano katika Kanisa ni Kiingereza, Kifaransa na Kireno, na sehemu kidogo mpenyezo wa Kiarabu. Sawia katika nyanja zingine za kisiasa, kiuchumi, kidiplomasia, kijamii. Bado watu ni wageni nyumbani. Swali mama, ni lini tutaacha kuwa wageni! Utamadunisho watutaka tutumie lugha ya nyumbani, si ya mgeni.

Hii ni hatua ya lazima katika utamadunisho. Shime wataalamu wetu na viongozi! Wayahudi hawachelei kutukumbusha unyeti wa kugenishwa, nao kule Babeli walilia na kunena: “Tuuimbeje wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni?”(Zab.137/(136):4). Mimi nawe tumwimbieje Bwana katika lugha ya kigeni? Jamani! Zeruzeru au wagonjwa wa ngozi wataisha tukiendelea kuwa wageni nyumbani; mafisadi watatutawala tukiendelea kubaki ugenini! Rushwa haitakoma, itabadili majina kadiri ya wakati na kula kwa zamu! Itakuwa zawadi, itakuwa tahania, itakuwa takrima, ....Utamadunisho ni sauti ya kinabii. Na sauti ya kinabii isikike katika lugha inayoeleweka. Tutweke mpaka kilindini, maana utamadunisho si vazi la kondoo.

Mapokeo (desturi: jambo la kawaida au linalotendwa kila siku; mazoea, ada, utamaduni, kanuni, mila: mambo yanayofanywa na sehemu kubwa ya jamii fulani yanayolingana na asili na utaratibu wa nyendo za jamii hiyo; desturi za jumla za jamii; mapokeo, mafundisho yaliyotokea zamani). Katika utamadunisho twahitaji kuyachunguza, kuyatafakuri na kuyainisha mapokeo. Mapokeo ya urithi wa kitume na mapokeo toka kwa babu zetu.

Ikiwa ubaguzi ni dhambi, hakuna mapokeo mema yatakayosema ubaguzi ni haki. Hapa ni lazima kuyachenga mapokeo yapate ladha ya Injili. Si ladha ya mazoea. Kumbuka ile Hotuba ya Mlimani (Mat.5-7). Kumbuka sehemu aliyosoma Yesu katika Sinagogo kutoka katika chuo cha nabii Isaya (Is.58:6; Lk.4:19). Ni vema sasa kuyaangalia majadiliano kati ya Yesu na Mafarisayo juu ya mapokeo (Mk.7:1-23; Mat.15:1-20; 23).

Katika kutamadunisha tutazingatia mapokeo haya: yanayojenga utawala wa Mungu; yanayothamini utu, uhuru na haki za binadamu. Madhali kipimo chetu ni Kristo, tujifunze maana ya maneno haya: “Nataka rehema, wala si sadaka”(Hos.6:6; Mat.9:13;12:7). Katika suala la mapokeo tafadhali tusichuje mbu na kumeza ngamia.

Madhehebu (fikira na mwongozo wa kidini unaotokana na uelewaji wake wa misingi ya dini hiyo na unaoleta tofauti ndogondogo za mawazo lakini zisizovunja misingi ya dini hiyo, wafuasi wa mawazo ya kiongozi wa dini, mwenendo fulani wa kufanyia au kuendeshea mambo) katika madhehebu tuna kanuni, taratibu, kaida ya dini, ibada, tambiko, unyago:mkutaniko wa wa watu mahali maalumu pa siri panapofundishwa mizungu ya mila za kabila kwa vijana, ngoma ya kuwafundisha wari mila za kabila zao; jando/majando: kumbi la watoto wanaume wanapotahiriwa na kufundishwa mambo yanayowahusu watakapokuwa watu wazima).

Binadamu kwa hulka ni mdini, binadamu asiyeamini ni pandikizo la ukoloni. Wataalamu wanakiri sasa kuwa mja ni mwamini Mwumba. Tofauti i katika namna ya kueleza hicho anachoamini. Petro hachelei kukiri: “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye”(Mdo.10:34-35).

Utamadunisho watutaka tuzitafakari, tuzichungue dini za asili na kuzifungamanisha na Injili, yaani kuziinjilisha na kuwa kielelezo halisi cha Mkristo mwafrika. (Kwa maneno ya Mtaalamu wetu: Kukristika kwa Mwafrika na kumwilika kwa Kristo ). Injili itwae mwili katika tamaduni za watu.

Na Padre Mayala Nikodemo,
Roma.










All the contents on this site are copyrighted ©.