Wazee ni tunu muhimu katika Jamii; wanapaswa kupokelewa, kuheshimiwa; wanateseka katika
ukiwa, wanapotengwa na kuelemewa na upweke
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu tarehe 12 Novemba 2012 ametembelea
nyumba ya wazee inayohudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kama sehemu ya maadhimisho
ya Mwaka wa Wazee Barani Ulaya na mshikamano kati ya kizazi na kizazi. Baba Mtakatifu
ametumia fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pamoja na Wasamaria wema
wanaoendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wazee wanaotunzwa
katika Jumuiya hiyo.
Baba Mtakatifu anasema, anawatembele kwa nafasi yake
kama Askofu wa Roma, lakini zaidi kama mzee mwenzao, anayefahamu fika matatizo na
changamoto zinazojitokeza katika umri kama huu na hasa zaidi wakati huu kutokana na
myumbo wa uchumi kimataifa, hali inayoweza kuwajengea kishawishi cha kutamani yale
yaliyopita wakati walipokuwa bado vijana, wakiwa na nguvu na mipango lukuki kwa siku
za usoni. Hali hii inaweza pia kuwajengea simanzi na huzuni. Licha ya matatizo na
changamoto wanazokabiliana nazo wazee sehemu mbali mbali za dunia, lakini, anapenda
kuwahakikishia kwamba, kwa hakika inapendeza kuwa mzee!
Kila umri una baraka
na utajiri wake na kamwe watu wasigubikwe na simanzi, kwani wamebahatika kupata maisha
marefu na kwamba, kuishi katika umri wao huo ni jambo jema kabisa, licha ya vizingiti
na vikwazo vinavyoweza kujitokeza, lakini wanapaswa kutambua kwamba, kweli wanapendwa
na Mwenyezi Mungu, hivyo, hakuna sababu ya kujawa na majonzi.
Katika Biblia
anasema Baba Mtakatifu, maisha marefu yalihesabiwa kuwa ni baraka kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, inayopaswa kupokelewa kama zawadi, kwa kuthaminiwa na kutunzwa. Wazee ni tunu
muhimu sana katika Jamii na wala si watu wanaopaswa kubezwa. Wazee wanateseka pale
wanapotengwa, wanapoishi mbali na nyumba zao na zaidi sana wanapojikuta wakielemewa
na upweke.
Baba Mtakatifu anashauri kuanza jitihada zitakazoziwezesha Familia
kuweza kuwatunza wazee nyumbani mwao, ili waweze kujichotea hekima, ujuzi, maarifa
na mang'amuzi waliojitwalia katika hija ya maisha yao. Ubora wa maisha ndani ya Jamii
husika unapimwa na jinsi ambavyo Jamii hiyo inawatunza na kuwajali wazee wake, kwani
hawa ni watu ambao wana hekima na hivyo utajiri wanaoubeba ndani mwao, hauna budi
kuthaminiwa. Jamii inayotoa nafasi kwa wazee, hiyo itambue kwamba, inapokea zawadi
ya maisha.
Baba Mtakatifu anaishukuru kwa namna ya pekee, Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwahudumia wazee na watu mbali mbali wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, ili kutambua kwamba, Kanisa ni kielelezo cha mshikamano na watu
wa vizazi vyote unaofumbatwa katika upendo. Thamani ya maisha na utu wa mwanadamu
havipungui kwa uzee, kwani kila mtu katika umri mbali mbali amenuiwa na kupendwa na
Mwenyezi Mungu, kumbe, ana maana na umuhimu wake.
Baba Mtakatifu anasema katika
maadhimisho ya Mwaka wa Wazee anapenda kusisitiza kwamba, wazee ni tunu muhimu sana
katika maisha ya Jamii, hasa zaidi kwa vijana, kwani wazee ni sawa na kitabu ambacho
kiko wazi, na vijana wa kizazi kipya wanaweza kupata miongozo ya maisha. Katika uzee,
mtu atatendewa hata kinyume cha utashi wake, kiasi cha kutolea ushuhuda wa maisha
yake, lakini wamshukuru Mungu pia kwa huduma inayotolewa na jirani zao, kwani kila
mtu anamtegemea mwingine, ili kujenga na kuimarisha mfumo wa Familia inayojengeka
katika upendo.
Baba Mtakatifu anawaambia wazee wenzake kwamba, kuna wakati
wanajisikia kwamba, muda wao hauna maana tena, umesheheni utupu na matatizo, hakuna
watu wa kukutana nao wala mambo wanayopaswa kutekeleza, haya yote yasiwakatishe tamaa;
hata pale wanapokabiliana na magonjwa na mateso, daima wakumbuke kwamba, maisha ni
zawadi ili kujenga na kuimarisha uhusiano na Mwenyezi Mungu. Mwenyeheri Yohane Paulo
wa pili hadi leo hii ni mfano na kielelezo cha kuigwa.
Baba Mtakatifu anawahimiza
wazee kuendelea kusali kwa imani bila kuchoka, kuliombea Kanisa na viongozi wake,
mahitaji ya dunia na maskini, ili haki na amani viweze kutawala duniani. Sala ya wazee
inaweza kuilinda dunia. Baba Mtakatifu amewakabidhi wazee hao jukumu la kuliombea
Kanisa na amani duniani. Watambue kwamba, anawapenda na kuwajali, kama wanavyopendwa
pia na Mwenyezi Mungu, wasikatishwe tamaa na ubinafsi unaojitokeza ulimwenguni kwa
kujali zaidi tija.