Kazi ni wajibu na utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ijikite daima kutafuta
mafao ya familia
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican uliyebahatika kufuatana nami toka mwanzo, utakumbuka
kuwa tumefanya tafakari ya kina kuhusu asili ya ndoa na familia kama ilivyo kwenye
Maandiko Matakatifu na kama Mababa wa Kanisa walivyofundisha kwa nyakati mbalimbali
bila kuyatupilia mbali mawazo mazuri ya wana taalimungu wa nyakati zetu. Nakualika sasa
kwa vipindi vichache vijavyo tuchukue mtazamo mwingine tupime uwiano uliopo kati ya
familia na kazi au kazi na mwanadamu. Katika kipindi chetu hiki cha kwanza, tukumbushane
tena kuwa: kazi ni wajibu au wito ambao chimbuko lake ni Mwenyezi Mungu katika uumbaji.
Wajibu huu wa kazi amekabithiwa mwanadamu ambaye hawezi kufikirika nje ya familia. Masimulizi
yote mawili ya uumbaji yaani Mwanzo sura ya kwanza na ya pili mwanadamu aliyeumbwa
kwa sura na mfano wa Mungu amekathiwa kazi zote za uumbaji ili azifanye na kuziendeleza.
Ni katika maana hiyo, Mwenye heri Yohane Paulo II katika waraka wake Laborem
Exercens, Namba 1, anarudia kusema, mwanadamu aliye sura na mfano hai wa Mungu
katika ulimwengu huu amekabidhiwa ulimwengu na yote yaliyoko ndani yake ili ayamiliki
na kuyatiisha katika maana hii ameitwa kufanya kazi. Kazi ndicho kipimo cha utu, kipimo
cha ubinadamu mwenye mahusiano na binadamu mwingine. La msingi hapa ni kuwa kazi
inafanywa na mwanadamu kwa ajili ya mwanadamu. Kazi sio matokeo ya adhabu ya dhambi
ya asili kwani mwaliko wa kufanya kazi ulishakuwepo hata kabla mwanadamu hajaanguka
dhambini. Japo matokeo ya dhambi huonekana katika ugumu wa kazi na matumizi mabaya
ya maana ya kazi. Ni katika maana hii, Bwana wetu Yesu Kristo alifanya kazi ili kuipa
tena kazi heshima yake iliyokuwepo tangu uumbaji. Kazi inapaswa kuwa kwa lengo la
kumsaidia mwanadamu na sio mwanadamu ageuke kuwa mtumwa wa kazi. Mahusiano yake na
mwanadamu mwingine yasigeuke kuwa chukizo badala ya furaha. Ndugu msikilizaji,
jukumu la ubaba, umama na hata nafasi ya utoto katika familia hudai wajibu fulani,
mmoja kwa mwingine, hudai mahusiano na bila mahusiano hayo ya kikazi usitawi wa kifamilia
hudumaa na hata kufa. Bila kazi familia hukosa maendeleo yake ya kiroho na kimwili,
ni ukweli kuwa wakati mwingine umasikini huzaliwa na hata kulelewa na uvivu. Ndugu
msikilizaji hapa nakualika turejee tena mwaliko wa Mtakatifu Paulo anayesema mtu asiyefanya
kazi hana ruksa ya kula chakula ( 2 Kol 3:1-13). Hata hivyo kazi ilete mahusiano mazuri
na isiwe sababu kumgeuza mwanadamu mtumwa wa kazi na kuharibu mahusiano mazuri na
mwanadamu mwingine. Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Raphel Mwanga,
wa Jimbo Katoliki la Same, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano-
Roma.