Jubilee ya miaka 100 ya Ukristo na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zake
nchini Nigeria
Askofu mkuu Anthony John Valentine Obinna wa Jimbo kuu la Owerri, Nigeria, anamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa namna ya pekee kwa kuwajalia waamini wa Jimbo lake kuweza kuadhimisha
Jubilee ya Karne moja tangu waliposikia Habari Njema ya Wokovu, tukio ambalo limewafungulia
pia maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita.
Waamini wa Jimbo kuu la Owerri walihubiriwa kwa mara ya kwanza
na Wamissionari wa Shirika la Roho Mtakatifu, maarufu kama Holy Ghost, wakitokea eneo
la Alsace-Lorraine. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, idadi kubwa ya wamissionari
waliwasili nchini Nigeria, wakapandikiza mbegu ya Ukristo, wakaipalilia na sasa katika
kipindi cha miaka mia moja imezaa matunda ya idadi kubwa ya Wakristo ambao ni imara
katika imani yao, licha ya patashika nguo kuchanika zinazojitokeza hapa na pale. Jimbo
kuu la Owerri kwa sasa lina idadi kubwa ya Mapadre na Watawa, kiasi kwamba, linaendelea
kushiriki katika kazi ya kimissionari ndani na nje ya Bara la Afrika.
Padre
wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Owerri, alipadrishwa kunako mwaka 1937 na wa pili alipadrishwa
kunako mwaka 1945, hawa ni zawadi kubwa na chemchemi ya miito Jimbo Kuu la Owerri,
kwani katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilee, jumla ya Mashemasi ishirini na wanne
wamepewa daraja takatifu la Upadre.
Askofu mkuu Obinna anasema kwamba, maadhimisho
ya Jubilee ya Karne Moja ya Ukristo Jimbo kuu Owerri ni fursa ya pekee, kuweza kukumbatia
na kumwilisha changamoto na fursa mbali mbali, zinazoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, katika: kuiungama imani, kuiadhimisha kwa uchaji mkubwa,
kuimwilisha katika maisha kwa kuongozwa na Amri za Mungu pamoja na kuhakikisha kwamba,
waamini wanaisali kama njia ya kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Kristo pamoja
na jirani zao, kwa sifa na utukufu wa Mungu.
Jimbo kuu la Owerri nchini Nigeria
linatambua changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya
sayansi na teknolojia, inayoufanya ulimwengu kuwa kama kijiji; wanatambua kwamba,
kuna tabia ya ukanimungu na watu kupenda mno malimwengu, mwaliko kwa waamini kuyatakatifuza
malimwenmgu haya, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Daima
wajitahidi kutangaza Ufalme wa Mungu unaojengeka katika misingi ya haki, amani, upendo
na mshikamano wa kweli. Wanahifadhi ndani mwao, ule Mwanga ambao ni Kristo mwenyewe
wanapopambana na malimwengu, ni matumaini yao kwamba, kwa kushikamana na Kristo katika
hija ya maisha yao hapa dunia, wataweza kuyashinda malimwengu.
Kwa upande wake,
Kardinali mteule John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, amemshukuru
kwa namna ya pekee Kardinali Fernando Filoni kwa kufika na kushiriki katika shamra
shamra za maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya Jimbo kuu la Owerri.
Anasema,
kwa kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuwa Kardinali ni
changamoto kwake binafsi kuendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtumikia
Mungu na Kanisa, akimsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kuwaongoza Watu wa Mungu.