Jimbo kuu la Owerri, Nigeria lahitimisha Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu,
tarehe 10 Novemba 2012, alihitimisha maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia moja ya ukatoliki
Jimbo kuu la Owerri, nchini Nigeria kwa Ibada ya misa takatifu iliyohudhuriwa na sehemu
kubwa ya Familia ya Mungu nchini Nigeria. Ilikuwa ni nafasi ya pekee, kwa ajili ya
kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa wema na ukarimu ambao amewajalia
waamini wa Jimbo Kuu la Owerri katika kipindi cha miaka mia moja, tangu waliposikia
Injili ya Kristo ikitangazwa masikioni na mioyoni mwao kwa mara ya kwanza.
Kardinali
Filoni anasema, miaka mia moja si haba, hata kama ikilinganishwa na Makanisa ambayo
yalibahatika kuhibiriwa Habari Njema kwa miaka mingi iliyopita. Kanisa Katoliki Jimbo
kuu la Owerri bado ni changa, lina nguvu, ari na mwamko wa pekee, unaojionesha katika
ukarimu na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Maadhimisho haya ni muhimu kwa ajili
ya kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewakirimia zawadi ya imani kwa takribani miaka mia
moja iliyopita.
Ni imani ambayo imepokelewa, ikashuhudiwa, ikaadhimishwa na
kumwilishwa kwa moyo wa uchangamfu na watu wa nyakati zile. Hii ndiyo ile imani ambayo,
Kanisa limeendelea kuitangaza na kuirithisha kizazi baada ya kizazi.
Ni imani
ambayo imafumbata kwa namna ya pekee, Habari Njema ya Wokovu inayomwezesha mwamini
kukutana na Kristo Mkombozi wa dunia. Ni imani ambayo imepokelewa na Mitume, wakairithisha
kwa waandamizi wao na wale walioipokea wakaendelea kuishuhudia kwa uaminifu mkubwa
kwa njia ya maisha yao. Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya waamini wa Jimbo kuu
la Owerri, nchini Nigeria, wakati huu wanapoanza ukurasa mpya baada ya maadhimisho
ya Jubilee ya miaka mia moja ya Ukristo Jimboni mwao.
Kardinali Fernando Filoni
aliwaalika waamini kusali kwa ajili ya kumshukuru pia Bikira Maria, Mama wa Kanisa
na nyota ya Uinjilishaji Mpya, ambaye daima amekuwa ni kielelezo makini cha imani
na ufuasi wa Kristo, ili aweze kuwasaidia kuwa kweli ni mihimili ya Uinjilishaji Mpya
katika: Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na waamini wa dini na madhehebu mbali
mbali kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kwani hii pia ni mbinu
mpya ya Uinjilishaji Mpya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Kardinali
Filoni anawaalika waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Injili
ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwani Uinjilishaji ni kielelezo cha upendo
wa dhati. Waamini wawe na ujasiri wa kushuhudia upya wa imani yao katika maisha yanayobubujika
kutoka kwa Kristo, ili waweze kweli kusimama kidete kutangaza na kushuhudia ujumbe
wa imani, matumaini na mapendo kwa Familia ya Mungu.