2012-11-12 08:26:18

Imani na upendo kwa Mungu na jirani ni chanda na pete!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa tafakario yake, Jumapili tarehe 11 Novemba, 2012 alifanya rejea kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini na mbili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwa kuainisha jinsi ambavyo wanawake wawili wajane walivyoshuhudia imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu. Wa kwanza ni yule mwanamke anayesimuliwa kwenye Somo la kwanza aliyetoa chakula chake chote kwa Nabii Eliya wakati akitambua kwamba, walikuwa wanakabiliwa na baa la njaa.

Ukarimu wake, ulimwonjesha huruma na upendo wa Mungu kiasi kwamba, ule unga na kiasi kidogo cha mafuta kilichokuwepo kamwe havikuisha hadi pale mvua ilipoanza kunyeesha tena. Katika Injili, Yesu anatambua majitoleo ya mwanamke mjane, aliyetumbukiza senti yake ya mwisho aliyokuwa ameificha kibindoni, wakati ambapo kulikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wanatoa ziada ya mali yao.

Ujumbe mkubwa wa Neno la Mungu katika matukio haya ni kwa waamini kujenga na kuyasimika maisha yao katika Neno la Mungu pamoja na kujiaminisha kwake. Wajane katika Maandiko Matakatifu ni watu waliokuwa wanateseka na kudhulumiwa katika Jamii zao, lakini Mwenyezi Mungu ni mtetezi wa yatima na wajane kama inavyojidhihirisha katika Maandiko Matakatifu, anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Haitoshi tu kuwa mjane, bali Mwenyezi Mungu anachotaka kwa kila mwamini ni uhuru binafsi, utakaomwezesha mwamini kujishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani. Wanawake wajane wanaosimuliwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya thelathini na mbili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, wanaonesha kwa namna ya pekee, upendo wao kwa Mungu na jirani. Hakuna mtu ambaye ni maskini kiasi kwamba, hana chochote cha kuweza kumtolea Mwenyezi Mungu; kwani Imani na Mapendo kwa Mungu na Jirani ni chanda na pete!

Papa Gregori mkuu anasema kwamba, katika mizani ya haki ya Mungu, kinachoangaliwa zaidi si wingi, bali uzito wa moyo wa mwanadamu, kama inavyojionesha kwa yule mwanamke mjane aliyetoa senti kidogo, akaonja huruma ya Mungu. Bikira Maria anasema Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, ni kielelezo kamili cha mtu anayejitolea bila ya kujibakiza akijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa imani hii, ndiyo maana alithubutu kusema, "Mimi hapa" kwa kuyapokea na kuyatekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu aliyageuzia mawazo yake kwa Mwenyeheri Maria Luisa Prosperi aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 10 Novemba 2012, Jimboni Spoleto-Norcia, Italia, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi hii kubwa ya Mwenyeheri Maria Luisa Prosperi, aliyeyahusisha maisha yake na mateso ya Kristo.

Jumapili iliyopita, Kanisa nchini Italia limeadhimisha Siku ya Shukrani kwa Mwenyezi Mungu ambayo katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kutenda mema, ili waweze kuirithi nchi. Huu ni mwaliko wa kuchuchumilia imani katika maisha, ili kutambua kwa moyo wa shukrani kazi ya upendo wa Mungu unaowalisha watoto wake. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasalimu kwa namna ya pekee, wakulima nchini Italia.

Jumapili iliyopita Poland pia imeadhimisha Siku kuu ya uhuru wake, kwa waamini kuwakumbuka waasisi wa imani, historia yao na moyo wa vijana wa kizazi kipya; mambo msingi ambayo wanapaswa kuyatumia kwa ajili ya kujenga msingi wa nchi yao. Amewapongeza kwa kuonesha mshikamano wa hali na mali kwa wakristo walioko Misri, walipokuwa wanaadhimisha Siku ya mshikamano na Makanisa yanayokumbana na dhuluma sehemu mbali mbali za dunia







All the contents on this site are copyrighted ©.