2012-11-12 09:21:14

Bibi Theresia Nago aomboleza kifo cha mtoto wake Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na mamia kwa mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki kumzika Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga yaliyofanyika kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, Parokia ya Ngokolo, mjini Shinyanga.

Rais Kikwete ambaye amekwenda Shinyanga akitokea Dodoma ambako anaendesha vikao muhimu vya Chama cha Mapinduzi amewasili kwenye Kanisa hilo kiasi cha saa sita mchana kwa ajili ya mazishi ya Askofu Balina ambaye alifariki dunia Novemba 6 mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa, Mwanza kwa ugonjwa wa saratani.

Mara baada ya kuwasili Kanisani hapo, Rais Kikwete ametia saini kitabu cha maombolezo na kujiunga na viongozi wa Kanisa hilo na wa Serikali akiwamo Rais Mstaafu Mheshimiwa Banjamin Mkapa na Mama Maria Nyerere kushiriki katika mazishi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.

Kabla ya kutoa salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesikiliza salamu za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, na pia amesikiliza Waraka uliotangaza kuteuliwa kwa Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Shinyanga hadi atakapoteuliwa Askofu mpya wa jimbo hilo.

Waraka huo umetolewa na kutiwa saini na Askofu mkuu Protas Rugambwa, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na kusomwa na Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini tanzania.

Katika salamu zake zake za rambirambi ambazo amezielekeza kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na waamini wa Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amemwelezea Askofu Balina kama kiongozi mwadilifu na mchapakazi ambaye hukuchoka katika maisha yake kutumia nafasi zake mbali mbali alizozishikilia katika maisha yake kuwasaidia binadamu wenzake.

Rais Kikwete pia ameelezea jitihada ambazo yeye na Askofu Balina walizifanya katika kusaka fedha za kupanuliwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko Mwanza.

Baada ya kutia udongo kwenye kaburi la Askofu Balina na kuweka shada la maua kwenye kaburi hilo, Rais Kikwete alimpa pole na kumfariji Bibi Theresia Nago ambaye ni Mama yake mzazi Askofu Balina kabla ya kuondoka Kanisani hapo.

Askofu Balina alikuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga nafasi aliyoishikilia kwa miaka 16 na kabla ya hapo alikuwa Askofu wa Jimbo la Geita kwa miaka 12. Askofu Balina alikuwa askofu kwa miaka 28 na Padre kwa miaka 41. Aidha, Askofu Balina alikuwa Mkuu wa Idara ya Afya ya TEC kwa miaka mingi na pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Bugando.









All the contents on this site are copyrighted ©.